Kikosi-cha-Serengeti-Boys-Under-20

TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys  imelazimisha suluhu pacha ya bila kufungana dhidi ya  Afrika Kusini, (Amajimbo) katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika za vijana.
Mchezo huo ulipigwa jana katika dimba la kisasa la Azam Complex, Chamazi, , Mbande, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, dakika 20 za kwanza, Afrika kusini walitawala na kulisumbua lango la Serengeti Boys, lakini mchezo huo ukabadilika na vijana wa Tanzania kuanza kusakata soka la uhakika.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Serengeti walipata nafasi mbili za wazi, lakini washambuliaji wake walishindwa kuzibadili kuwa magoli.
Na katika kipindi cha pili, Serengeti walionekana kuwa na bahati kwasababu walitengeneza nafasi nyingine mbili za wazi, lakini washambuliaji walikosa umakini.
Kilichoonekana kwa vijana wa Tanzania ni kuwa na uoga, lakini kadiri dakika zilivyozidi kukata walitulia na kuweka akili mchezoni. Kwa Amajimbos walionekana kuwa imara na bora kiufundi, hivyo mchezo wa marudiano kule Bondeni utakuwa mgumu kwa Serengeti Boys.
Kwa matokeo hayo, kocha mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali ana kazi ya kujiandaa vizuri kwasababu atahitaji ushindi ili kuwatoa wenyeji kule Afrika kusini au sare ili ya mabao yoyote, kwa maana ya kufaidika kwa mabao ya ugenini.
 
Top