DSC_0027
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Ratiba ya ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2014/15 tayari ipo wazi. Septemba 20, timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa viwanjani kukata utepe. Mechi inayotaraji kuwa kali zaidi siku ya ufunguzi ni ile kati ya mabingwa mara mbili wa zamani, Mtibwa Sugar dhidi ya mabingwa mara 24 wa kihistoria Yanga SC katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Mechi kati ya Mtibwa na Yanga katika uwanja huo imekuwa ngumu kwa timu hiyo ya Dar es Salaam ambayo itakuwa ikisotea ubingwa wa kwanza katika kipindi cha miaka mitano katika uwanja huo.
Yanga imekuwa ikiichapa Mtibwa katika uwanja wa Taifa, lakini hali imekuwa tofauti kila wanapotua uwanja wa Jamhuri huku wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 3-0, 19 Septemba,  2012.
Mabingwa watetezi Azam FC wataanza utetezi wao dhidi ya timu ya Polisi Morogoro ambayo imerejea katika ligi kuu baada ya kushuka daraja mwaka mmoja uliopita. Mechi hiyo itakuwa ngumu kama ilivyokuwa katika ligi ya msimu wa 2012/13 wakati timu hizo zilipotoshana nguvu katika michezo yote miwili.
Mbeya City ambao walipoteza mchezo mmoja tu katika uwanja wa nyumbani msimu uliopita, wataanza msimu wao wa pili katika ligi kuu Bara kwa kuwakaribisha JKT Ruvu ambao imefanya usajili wa wachezaji ‘ lukuki’ kutoka klabu za Mtibwa, Simba, Yanga na timu nyingine. JKT Ruvu imemrejesha kocha wake wa zamani, Fred Minziro ambaye alikijenga kikosi hicho miaka ya nyuma na kufanikiwa kushinda ubingwa wa Kombe la Taifa ‘ Kaombe la FAT’ na kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya kombe la washindi mwaka 2002.
City iliyochini ya Juma Mwambusi ilimaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita na haijafanya usajili wowote mkubwa kwa kuwa tayari kikosi hicho kilikuwa na wachezaji wa kutosha ambao wameonekana kuimarika katika msimu wao wa kwanza tu, lakini dhidi ya JKT Ruvu ya Minziro inaweza kuwa mechi ngumu kwa kila upande nap engine City wanawqeza kupoteza mchezo huo wasipokuwa makini.
Washindi wanne msimu uliopita, Simba wataanzia ugenini siku ya Jumapili, 21 Septemba kwa kucheza na Coastal Union. Simba ililazimisha suluhu katika uwanja wa Mkwakwani msimu uliopita ila ilichapwa bao 1-0 katika uwanja wa Taifa wakati wa mchezo wa marejeano.
Ratiba safari hii imepangwa vizuri, na timu zitacheza kila mwisho wa wiki kwa miezi saba mfululizo hadi 18 April, 2014. Licha ya kuwepo na michezo mingi ya upinzani na ile ambayo itahusisha timu kali kwa kipindi chote cha msimu. Zifuatazo ni mechi saba kali zaidi ambazo zitahusisha timu hasimu katika mkoa mmoja ‘ Derby’ au ‘ Pacha’ kwa lugha ya Kiswahili.
11 OKTOBA, 2014
POLISO MORO vs MTIBWA SUGAR
Mechi hii itazihusisha timu mbili za Mkoa wa Morogoro ambazo zinatoka katika maeneo tofauti ndani ya mkoa huo. Polisi wanatoka katikati ya mji wa Morogoro, kwa maana nyingine ni ‘ timu ya mjini’ huku Mtibwa Sugar ikitoka nje ya mkoa huo, Turiani, Morogoro. Mtibwa ipo chini ya Mecky Mexime ambaye huu utakuwa msimu wake wa tatu mfulilizo huku Polisi ikiwa chini ya mwalimu mzoefu Adolf Richard ambaye amekuwa na timu hiyo tangu Disemba, 2012.
Polisi imefanya maboresho makubwa katika kikosi chake kwa kuwasaini wachezaji wazoefu kama mlinzi Lulunga Mapunda, huku Mtibwa ikifikiria namna ya kuziba nafasi za wachezaji JUma Luizio aliyeuzwa kwa Zesco United ya Zambia na golikipa, Hussein Shariff aliuzwa kwa Simba. Ni moja ya mechi ngumu katika wiki ya nne ya ihasisha timu ambazo hazikufunga katika michezo yote miwili, msimu wa 2012/13. Mechi hii itapigwa katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
COASTAL UNION vs MGAMBO JKT
Timu mbili za Tanga zitapambana zenyewe kwa zenyewe katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Itakuwa mechi ya tatu kwa kila timu katika uwanja wa nyumbani, Coastal baada ya kucheza na Simba watasafiri hadi Mbeya kucheza na Mbeya City katika wiki ya pili. WAtaikabili Mgambo wakiwa wametoka kucheza na Ndanda FC ya Mtwara katika wiki ya tatu. Chini ya kocha Mkenya, Yusuph Chippo ‘ Wagosi wa Kaya’ wamejiimarisha kwa kuongeza nguvu ya wachezaji wengi chipukizi kutoka timu yao ya pili ambayo imekuwa na mafanikio makubwa katika miaka miwili ya karibuni. Golikipa, Shaaban Kado anatarajiwa kuwa mchezaji muhimu zaidi wa mabingwa hao wa mwaka 1988.
Mgambo itacheza ligi kuu kwa msimu wa tatu mfululizo na mara zote mbili timu hiyo imenusurika kushuka dakika za mwisho. Mohammed Samatta alifanya vizuri msimu uliopita akicheza sehemu ya kiongo, Mohammed Netto ni baadhi ya wachezaji ambao wanatarajiwa kukinyanyua kikosi hicho ambacho kilipoteza mchezo mmoja mbele ya mahasimu wao msimu uliopita. Mgambo wamekuwa wagumu kwa Coastal kiasi cha kufufua upinzani wa soka katika mkoa huo wa Kaskazini mwa Tanzania. Zamani ilikuwa ni Coastal Union v Africans Sports, lakini mechi hiyo imepotea na imegeuka, Coastal vs Mgambo kama mechi kali mkoani humo.
YANGA SC vs SIMBA SC
Mechi kali zaidi katika wiki ya nne ni hii ambayo itawahusisha mahasimu wa soka la Tanzania hata kabla ya uhuru. Yanga watakuwa wenyeji wa Simba katika uwanja wa Taifa na timu hizo zilitoka sare katika michezo yote miwili msimu uliopita. Timu zote zitakuwa na makocha wapya, huku mabadiliko ya wachezaji pia yakiwepo kila upande. Gelson Santos ‘ Jaja’, Andrey Coutinho ni baadhi ya wachezaji wapya na wachezaji hao wametoka Brazil wakiambatana na kocha Marcio Maximo.
Patrick Phiri amerejea tena klabuni Simba baada ya kuondoka miaka mitatu iliyopita, ameambatana na wachezaji kadhaa wapya katika timu hiyo ambao watakutana na mchezo wa kwanza wa mahasimu katika wiki ya nne tu. Pierre Kwizera  na Hussein Butoyi kutoka Burundi, Paul Kiongera kutoka Kenya, na wachezaji wazawa kama Manyika Peter ,Manyika, Hussein Shariff, Mohammed Hussein, Abdi Banda, Elius Maguli, Shaaban Kisiga na wengine.
Simba ilitoka nyuma ya mabao 3-0 na kutumia dakika 45 za kipindi cha pili kusawazisha mabao yote na kulazisha sare ya kufungana mabao 3-3, 20 Oktoba, 2013 katika mchezo wa kwanza msimu uliopita. Saimon Msuva aliisawazishia timu yake ya Yanga dakika za majeruhi katika mchezo wa marejeano, 24 April  mwaka huu wakati timu hizo zilipofungana  bao 1-1. Yanga haijafungwa na Simba katika misimu miwili mfululizo na kama wanahitaji kuendeleza hilo ni lazima wapambane zaidi siku hiyo. Mara ya mwisho Simba kuifunga Yanga katika ligi kuu ilikuwa, 7 May, 2012 waliposhinda kwa mabao 5-0.
8 NOVEMBA, 2014
JKT RUVU vs RUVU SHOOTING
JKT Ruvu hutumia uwanja wa Azam Complex Chamanzi kama uwanja wake wa nyumbani, Shooting hutumia uwanja wa Mlandizi, Mabatini, Pwani kama uwanja wake wa nyumbani lakini mechi baina ya timu hizo huwa na kisasi kisichokwisha. Timu hizo zote zinatoka eneo la MLandizi, na zinamilikiwa na jeshi . JKT Ruvu awali ilikuwa ni Shooting lakini mara baada ya timu hiyo kupanda ligi daraja la kwanza mwanzoni mwa miaka ya 2000, marehemu Meja, Jackson Lema aliamua nafasi hiyo wapewe JKT Ruvu na Shooting ikaanza tena ligi daraja la nne hadi ilipopanda katikati ya miaka 2000 katika ligi kuu Bara kwa mara ya kwanza kabla ya kushuka.
Shooting itakuwa katika msimu wake wan ne mfululizo wa ligi kuu tangu walipopanda kwa mara ya pili na timu hiyo imekuwa ‘ mwiba’ mkali kwa JKT Ruvu kila wanapokutana. Februari mwaka huu Shooting iliichapa JKT Ruvu kwa mabao 2-0 katika uwanja wa Chamanzi na haikupoteza mchezo dhidi ya mahasimu wao msimu uliopita kwa kuwa mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare mwezi Septemba, mwaka jana. Zitakutana katika uwanja wa Chamanzi katika mchezo wa raundi ya nane. Shooting ipo chini ya kocha raia wa Kenya Tom Olaba ambaye alichukua nafasi ya Boniface Kwassa, Disemba, 2013.
YANGA SC vs AZAM FC
Timu hizo zitakutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii kabla ya kuanza kwa msimu mpya. Azam itakuwa wageni wa mchezo huo na wataingia uwanjani wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya Yanga katika ligi Walichapa Yanga mabao 3-2  katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu uliopita, na kulazisha sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa marejeano . Wameongeza nguvu katika kikosi chao kwa kusajili wachezaji kama Mhaiti, Leonel Saint, Mrundi, Didier Kavumbagu ambaye aliichezea Yanga kwa misimu miwili, Ismail Diarra kutoka Mali.
Yanga hawatataka kupoteza lakini hawatazuia hali hiyo kama hawatakuwa makini na kikosi hicho cha kocha Patrick Omog. Itakuwa mechi ya mzunguko wa nane  ligi ikiwa imeanza kuchanganya. Azam wanatoka nje ya mji wa Dar es Salaam, wakati Yanga wanatoka katikati ya jiji. Ni mechi kali zaidi katika raundi hii ambayo itahususha timu mbili za Dar es Salaam ambazo zilimaliza katika nafasi mbili za juu msimu uliopita.
1 JANUARI, 2015
AZAM FC vs SIMBA SC
Azam hutumia uwanja wake wa nyumbani Chamanzi ila kutokana na wingi wa mashabiki wa klabu za Simba na Yanga mechi zao dhidi ya timu hizo kubwa nchini huchezwa katika uwanja wa Taifa. Watarudi tena katika uwanja wa Taifa siku ya mwaka mpya, safari hii wakiwa wenyeji wa Simba SC. Azam ilifunga Simba katika michezo yote miwili msimu uliopita.
Walishinda kwa mabao 2-1 katika kila mchezo ila hawatapata nafasi hiyo tena kama wataingia uwanjani wakitegemea uwezo uliopita. Simba imejipanga na inataka kuhakikisha wanafanya vizuri msimu ujao ili kufuta ‘ jinamizi’ la misimu miwili lakini hawatafanikiwa kama watashindwa kupata matokeo dhidi ya timu zinazowania ubingwa kama ilivyokuwa msimu uliopita waliposhindwa kupata ushindi katika michezo sita dhidi ya timu za Azam FC, Mbeya City na Yanga ambazo zilimaliza katika nafasi tatu za juu. Mechi hii itapigwa katika wiki ya 12 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
MBEYA CITY vs TANZANIA PRISONS
Machi 30, 2014, Mbeya City iliichapa Tanzania Prisonsi kwa bao 1-0 katika mchezo ambao ulitawaliwa na purukushani kubwa. Timu hizo za Mbeya zilikuwa na uhasama mkubwa msimu uliopita na mchezo wao wa kwanza uliomalizika kwa sare ulikuwa na vurugu kubwa huku vitendo visivyo vya kiungwana vikitawala ndani na nje ya uwanja. Baadae kulizuka vurugu kubwa ambazo jeshi la Polisi lilipambana nazo laki hali ni shwari hivi sasa baada ya kila upande kuahidi kuendelezea upinzani wao ndani ya uwanja .
Timu hizo zote zinanolewa na makocha wazawa wa mkoa huo, Juma Mwambusi kwa upande wa City na David Mwamaja kwa upande wa Prisons. Mwamaja ameongeza nguvu kwa kumsaini mshambulizi, Amiry Omary ambaye amefanya vizuri katika misimu miwili iliyopita akiwa na kikosi cha JKT Oljoro. Wakati Azam na Simba wakipambana uwanja wa Taifa, katika uwanja wa Sokoine timu mbili hasimu za mkoa huo, Mbeya City na Tanzania Prisons zitakuwa zikipambana kuwania pointi tatu muhimu.

 
Top