1
WASHAMBULIAJI wawili wa kimataifa wa Tanzania wanaokipiga TP Mazembe ya DR Congo, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wataiongoza klabu yao dhidi ya mahasimu wao wa jadi,  AS Vita katika mchezo wa mwisho wa kundi A wa ligi ya mabingwa barani Afrika.
Kuelekea katika mechi hiyo atakayochezwa mjini Kinshasa, homa imepanda kwa mashabiki  wa klabu hizo ingawa zote zimefuzu kucheza nusu fainali, lakini heshima ndio kitu muhimu zaidi.
Mechi hiyo itaamua ni klabu gani imalize ya kwanza kundi A ambapo ni mara ya kwanza katika historia ya DR Congo kuona klabu mbili za nchi hiyo zikifuzu hatua ya nusu fainali ya ligi ya mabingwa.
Kitu cha pili, AS Vita wanataka kuhakikisha wanashinda dhidi ya Mazembe ili kuwapa raha mashabiki wake kwasababu wamefungwa mara mbili mfululizo.
Mazembe wanarudi katika dimba la Stade Tata Raphael ikiwa imepita miezi minne tangu waifunge Vita 1-0, mei 11 mwaka huu na kutwaa ubingwa wa ligi kuu, lakini kulitokea vurugu kubwa na kusababisha watu 15 kupoteza maisha.
Wakati huo huo Mazembe wanajipanga kuibuka na ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya AS Vita ili kumaliza kileleni katika kundi A na kucheza nusu fainali mwezi septemba.
Hata hivyo, wanakabiliana na Vita ambao wamepoteza mechi moja tu katika kundi A na wanakwenda kucheza mechi hiyo wakitokea kushinda bao 1-0 ugenini dhidi ya waburuza mkia wa kundi hilo, Zamalek,  Agosti 10 mwaka huu.

 
Top