Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Alikuja akaondoka bila kuaga, alirudi akaondolewa kwa sababu, sasa anarejea tena kwa mara ya tatu klabuni Simba SC kama mkufunzi mkuu wa idara ya ufundi. Namzungumzia, kocha raia wa Zambia, Patrick Phiri ambaye anatua nchi kesho akitokea kwao kujiunga na Simba kwa mara ya tatu katika kipindi cha miaka kumi’. Phiri ameandaliwa mkataba wa miaka miwili na atasaini mara baada ya kuafikiana kuhusu mambo binafsi.
Ni kocha mzuri ambaye wachezaji wengi hupenda kufanya naye kazi. Mahitaji ya lazima ya timu ni kupata ushindi kadri inavyotakiwa lakini hilo litawezekana kama mahusiano ya kijamaa yataboreshwa kati ya uongozi na kocha, kwa maana ya kumuachia majukumu yote ya ufundi mwalimu. Mara ya kwanza, Phiri aliondoka na hakutaka kurejea kuifundisha timu hiyo alipotwaa ubingwa wa Tanzania Bara mwaka, 2004 na ilikuja kugundulika kuwa mwalimu huyo alichukizwa na kitendo cha baadhi ya viongozi kumuingilia katika majukumu yake ya upangaji wa timu na kumchagulia wachezaji wa kuwatumia.
Tabia hiyo bado ipo na inaendelea kuwahukumu makocha wengi klabuni Simba na hata, Mcroatia, Zdravko Logarusic ameondoka kwa sababu hizo. Heshima ya mtu inategemea jitihada zake za ufanyaji wa kazi na kutimiza majukumu yake. Kupendana, kuheshimiana kindugu, viongozi wanatakiwa kuwaamini walimu ambao wamekuwa wakipewa kazi na kuwaacha wafanye kazi yao. Simba wanatakiwa kuishi maisha ya kijamaa ambayo kila mtu, mchezaji, kiongozi na benchi la ufundi anatakiwa kujua wajibu wake wa uwepo klabuni.
Anaijua Simba, amewahi kufanya kazi, na ana mafanikio makubwa, ni sababu tatu ambazo, Zacharia Hans Poppe amesema zimewashawishi kumrejesha kocha huyo bora wa Zambia, mwaka, 1999. Ni ukweli ulio wazi kuwa rekodi ya Phiri ndani ya uwanja ni bora pengine kuliko walimu wote ambao wamewahi kufanya kazi klabuni hapo. Phiri alichukua nafasi ya Mkenya, James Siang’a mwaka, 2004 na aliweza kuifanya timu hiyo kuwa imara katika mashambulizi huku akiwatumia wachezaji wa nafasi ya kiungo katika safu ya mashambulizi. Shaaban Kisiga, Athumani Machuppa, Nico Nyagawa, Mussa Hassan Mgosi nyota hao walikuwa wachezaji wa kutegemewa katika ufungaji.
Phiri ambaye amewahi kucheza michuano ya AFCON, 1978 na 1982 pia amewahi kushiriki michuano hiyo kama kocha mkuu wa Zambia, mwaka, 2008 nchini Ghana ni mtu asiyeishiwa sababu za kwenda nyumbani mara kwa mara hali ambayo imekuwa ikiathiri utendaji wa timu ndani ya uwanja. Mara ya mwisho alipoondoka klabuni, Simba alichukizwa na kitendo cha kuingiliwa katika majukumu yake na hivyo kuamua kutoongeza mkataba baada ya kufanya kazi kwa miaka miwili mfululizo na kuwa kocha aliyekaa kwa muda mwingi klabuni hapo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Trott Moloto alidumu kwa mwezi mmoja baada ya kuchukua nafasi ya Phiri mapema, 2005.
]