Nyota anayechipukia: Thibaut Courtois anatazamiwa kuanza dhidi ya Burnley.
THIBAUT Courtois ameshinda mbio za kuwa kipa namba moja wa Chelsea.
Mbelgiji huyo anatazamiwa kuanza mbele ya Petr Cech katika mchezo wa ufunguzi wa ligi kuu jumatatu usiku dhidi ya Burnley.
Maamuzi ya Jose Mourinho kumchagua kipa huyo mwenye miaka 22 badala ya Cech ambaye amekuwa kipa namba moja kwa muongo mmoja tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea Rennes, imeongeza mashaka juu ya hatima ya baadaye ya mchezaji huyo.
Paris Saint-Germain, Monaco na Real Madrid wote wanaonekana kuwa na nia ya kumsajili Cech.
Wanasubiri kuona maamuzi ya Mourinho ili kuanza harakati za kumnasa kipa huyo.
Courtois alikuwa akicheza kwa mkopo kwa misimu mitatu iliyopita katika klabu ya Atletico Madrid na alikuwa sehemu ya kikosi kilichozishangaza Real madrid na Barcelona na kutwaa ubingwa wa La Liga na kufika fainali ya UEFA.
Mourinho anaamini atawatumia makipa wote katika kampeni zake, lakini alikiri ijumaa kwamba mchezaji asipochaguliwa kama namba moja katika kikosi chake anatakiwa kuanza kuangalia hatima yake ya baadaye klabuni hapo.
Cech mwenye miaka 32 anaweza kuamua kukaa benchi katika mechi nyingi za msimu au kutafuta ukurasa mpya wa maisha yake ya soka katika klabu nyingine.