Ilikuwa
ni makosa makubwa kukubali sare dhidi ya Coastal Union, na imekuwa hivyo dhidi
ya Polisi Morogoro, ni makosa ambayo yatatugharimu sana. Lengo ni kupata
pointi zote tatu katika michezo ya mzunguko wa kwanza. Ligi ni ngumu, kila timu
imejiandaa. Tumefanya makosa katika safu ya ulinzi , ni wakati wa kuamka na
kufanya vizuri” ni maneno ya kocha wa Simba SC, Mzambia Patrick Phiri
mara baada ya timu yake kulazimishwa sare mara mbili katika michezo ya ligi kuu
Bara katika uwanja wa Taifa.
Kuna
kitu kama tabia ya kawaida kwa Simba SC kuongoza mchezo kisha kushindwa kupata
pointi tatu hasa katika miaka ya karibuni. Rekodi ya kwanza ni pale Mbeya City
ilipotumia dakika 45 za kipindi cha pili kusawazisha mabao ya Amis Tambwe
katika uwanja wa Taifa msimu uliopita. Simba ikiwa chini ya makocha Abdallah
King Kibadeni na Jamhuri Kiwelo ilipoteza uongozi wa mabao 2-0 na kulazimishwa
sare ya kufungana mabao 2-2 na City.
Huenda mashabiki wa Simba ‘ walichanganyikiwa’ wakati ule, kama wengi wao bado
bila shaka watakuwa katika hali hiyo hivi sasa wakati Ligi kuu Tanzania Bara
ikiwa katika wiki yake ya pili. Labda ni alama ya uhasama kati ya Simba na
Coastal Union ndiyo iliyofanya timu hiyo ya Tanga kutumia dakika 25 za mwisho
kupambana na kusawazisha mabao ya mapema ya Simba na kulazimisha sare ya
kufungana mabao 2-2 katika wiki ya kwanza, Coastal ilichapwa na Mbeya City
katika mchezo uliopita, lakini walihakikisha wanacheza soka la kushambulia
dhidi ya Simba kwa kuwa hawakuwa tayari kukubali kufungwa.
Donald
Mo
soti
Akifadhaishwa
na uchezaji wa safu yake ya ulinzi katika michezo miwili ya mwanzo msimu huu,
kocha wa Simba, Mzambia, Patrick Phiri amekiri kuwa timu yake ina tatizo kubwa
katika safu ya ulinzi. Kumbuka, Phiri alikubali kuachwa kwa mlinzi wa kati,
Mkenya, Donald Musoti na kukubali kusainiwa kwa kiungo-mshambulizi, Mganda,
Emmanuel Okwi siku ya mwisho ya usajili nchini. Mambo yamepamba moto sasa,
Hassan Isihaka ameaminiwa na Phiri kuliko, Joram Mvegeke na chipukizi huyo
amekuwa akicheza sambamba na naodha, Joseph Owino katika safu ya ulinzi wa
kati.
Phiri
anatakiwa kuwapandisha viwango wachezaji hao wasio na uzoefu, hiyo ni moja ya
sababu zilizomfanya awe kocha wa timu hiyo. Dakika 180 za kwanza zimeonyesha
wazi kuwa, Simba ilimuhitaji zaidi Musoti katika kikosi chake msimu huu kuliko,
Emmanuel Okwi, Paul Kiongera au Pierre Kwizera. Kumuacha mlinzi huyo mwenye
nguvu na anayesimama mbele ya golikipa wake na kuwachua wachezaji hao watatu wa
kimataifa hakukuonekana ni kosa kwa sababu mashabiki walipumbazwa na sifa
nyingi zilizotangazwa na vyombo vya habari kuhusu, Okwi, Kiongera na Kwizera.
Simba
itacheza mchezo wa tatu katika uwanja wa Taifa dhidi ya Ndanda, Phiri anatafuta
ushindi wa kwanza katika ligi kuu, wiki tatu baada ya kuishinda Gor Mahia ya
Kenya kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki. Timu ambayo
ilionekana kuwa na nguvu katika kipindi cha pili siku ya mchezo wa Gor Mahia
imekosa maarifa ya kulinda mabao yao dhidi ya timu za Coastal Union na Polisi
Morogoro ambao walisawazisha bao pekee la Simba, dakika tano baada ya kuanza
kwa kipindi cha pili.
Upinzani
wa ubingwa umekuwa mkali kuanzia misimu mitatu iliyopita wakati, Azam FC
walipowaangusha Yanga SC na kumaliza katika nafasi ya pili msimu wa 2011/12.
Simba ilipata ushindi katika mchezo mmoja tu wa ugenini msimu uliopita
walipoifunga, JKT Oljoro. Hawakupata ushindi katika michezo miwili dhidi ya
Tanzania Prisons na Mbeya City katika uwanja wa Sokoine, Mbeya. Waliambulia
pointi moja katika safari mbili katika uwanja wa Mkwakwani, Tanga,
walilazimisha suluhu-tasa dhidi ya Coastal Union na wakapoteza mbele ya Mgambo.
Kuonyesha
timu hiyo haikuwa na uwezo wa kugombea ubingwa iliambulia pointi mbili
iliposafiri kwenda Jamhuri, Morogoro na Kaitaba, Bukoba ambapo kote huko
walifanikiwa kuambulia sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa Sugar kisha Kagera
Sugar. Kilichowakera mashabiki wa timu hiyo msimu uliopita ni kutokana na
uongozi mbaya uliokuwepo, lakini chini ya ‘Mtu wa Pointi Tatu’ hali imeanza
kwenda vilevile msimu huu. Phiri alimaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote
miaka minne iliyopita
Huwezi
kucheza vizuri kila mechi, Phiri kama kocha mtaalamu wa mbinu anaweza kufanya
mabadiliko ya wachezaji, kubwa ni kuwafanya walinzi wake wawe na hali ya
kujiamini muda wote huku wakicheza kwa umakini zaidi. Timu yake imekuwa na
uwezo wa kufunga mabao huku wakicheza soka zuri kwa muda fulani wa mchezo.
Hakuna timu yenye nafasi nzuri tu ya kushinda mechi lakini, Mtibwa Sugar na
Azam FC wamefanikiwa kushinda michezo miwili ya mwanzo kwa kuwa wanacheza kwa
nidhamu, umakini na ushirikiano. Mtibwa na Azam wamecheza michezo yote miwili
katika viwanja vyao vya nyumbani, lakini Simba imeshindwa kufanya hivyo na
kinachowagharimu ni safu yao ya ulinzi.