Hakuna kujitetea:Kikosi cha Manchester United chini ya Louis van Gaal kina thamani inayofikia paundi milioni 379
LOUIS van Gaal hatakuwa na la kujitetea kama Manchester United itashindwa kupambana kusaka ubingwa msimu huu.
Hii inatokana na ukweli kwamba Van Gaal ndiye kocha mwenye kikosi ghali zaidi katika ligi ya England kwa sasa.
Baada ya usajili mkubwa majira ya kiangazi, tafiti zinaonesha kuwa bosi huyo wa United ana kikosi chenye thamani ya paundi milioni 379.4.
Thamani hiyo haifikiwi na Manchester City ya Manuel Pellegrini na Chelsea ya Jose Mourinho.
Tangu kustaafu kwa Sir Alex Ferguson mwaka mmoja uliopita kampeni za kuwania ubingwa ziliisha na United wamejaribu kutumia paundi milioni 215 kusajili wachezaji ili kurudi katika kiwango cha juu.
Katika dirisha la usajili majira ya kiangazi pekee, United wamevunja rekodi ya usajili nchini England kwa kuinasa saini ya Angel Di Maria.
Pia waliwasajili Ander Herrera, Luke Shaw, Marcos Rojo na Daley Blind kabla ya kutumia paundi milioni 5 nyingine kumchukua kwa mkopo Radamel Falcao kutoka Monaco.
Wakati Burnley walivunja rekodi yao ya usajili kwa kulipa dau la paundi milioni 3 kwa George Boyd, United wana wachezaji 16 ambao ada yao ilianzia angalau paundi milioni 10 kwenda juu.
Wakati kikosi kinakosolewa kuwa na wachezaji wengi wa safu ya ushambuliaji, Van Gaal atakuwa na mlinda mlango David de Gea na mabeki Phil Jones, Chris Smalling, Rafael, Rojo, Shaw na Blind – waliosajiliwa kwa dau la paundi milioni 104.7