IMG_0135
Kikosi cha Mtibwa Sugar kilichoizamisha Yanga mabao 2-0 jana uwanja wa Jamhuri Morogoro. (Picha kwa hisani ya Globalpublisher)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MARCIO Maximo aliwahi kumfundisha kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mexime kama ilivyo kwa makocha wengine ambao hupenda kuwaadhibu waalimu wao pale wanapokutana wakiwa na majukumu sawa, jana alifanikiwa kumtandika kwa mara ya kwanza Marcio Maximo mabao 2-0 akiiongoza Yanga.
Mbali na kumfunga mwalimu wake, Mexime ameweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kumfunga Maximo katika ngazi ya klabu nchini Tanzania, hivyo hatasahaulika kichwani mwa Mbrazil huyo mwenye mvuto mkubwa kwa Wanayanga.
Ilikuwa mechi ngumu kwa nahodha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Taifa Stars, lakini aliwashinda Yanga kwa ‘staili’ ya kutumia mipira mirefu ambayo mabeki wa Maximo wakiongozwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro; na Kelvin Yondani walishindwa kucheza vizuri.
Mtibwa wakiwa kwenye morali kubwa, vipindi vyote viwili walizidiwa na Yanga katika kumiliki mpira, lakini walikuwa na hesabu kali kila walipofika langoni.
Kipa Said Mohamed aliyewahi kuichezea Yanga akitokea Maji Maji fc ya Songea ‘Wanalizombe’ aliokoa michomo ya hatari langoni kwake na pengine kwa mtazamo wa wengi ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi.
Mohamed akiwa katika kiwango cha juu, aliwanyima nafasi Yanga kugusa nyavu zake, ingawa Geilson Santos Santana ‘Jaja’ na Saimom Msuva walifunga magoli mawili ambayo yalikataliwa na mwamuzi Dominick Nyamisana wa Dodoma.
Dakika ya kwanza tu ya kipindi cha pili, beki wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde alinawa mpira akiwa eneo la hatari na mwamuzi kuizawadia Yanga penalti, licha ya kwamba Jaja tayari alikuwa amekwamisha gozi kambani.
Jaja akiwa amebeba matumaini ya Wanayanga wengi waliofurika uwanja wa Jamhuri alikosa penalti hiyo kufuatia kipa Mohamed kupangua kwa mguu wake wa kushoto.
Kocha Mexime wa Mtibwa, hakuwa na maneno mengi kama ilivyo kawaida yake.
Akijiamini kuwa kikosi chake kimefanya vizuri zaidi ya kile cha bosi wake wa zamani, Maximo, Mexime alisema: “Namshukuru Mungu kwasababu wachezaji wangu wamejituma na kufanya kazi tuliyowatuma”.
“Tunajiandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Ndanda fc nyumbani, hivyo tumeanza maandalizi baada ya kumaliza kazi hii ngumu mbele ya Yanga”.
Septemba 27, Mtibwa Sugar wataikaribisha Ndanda fc katika uwanja wake wa katikati ya miwa, Manungu Complex.

 
Top