Maswahiba: Rais wa Real Madrid, Florentino Perez ameitete sera ya usajili ya kalbu hiyo baada ya maoni ya Cristiano Ronaldo
RAIS wa Real Madrid, Florentino Perez ameitetea sera ya klabu yake ya usajili baada ya Cristiano Ronaldo kufunguka ya moyoni akipinga kuuzwa kwa Angel di Maria katika klabu ya Manchester United kwa dau la paundi milioni 60.
Mabingwa hao wa Ulaya pia walimuuza kiungo wa kimataifa wa Hispania Xabi Alonso katika klabu ya Bayern Munich kwa dau la paundi milioni 5, kitu ambacho kimemvunja moyo Ronaldo ambaye aliponda waziwazi maamuzi ya Perez.
Lakini Perez alisisitiza kuwa hakuna tatizo akisema: “Namjua vizuri Cristiano Ronaldo. Cristiano ni mchezaji bora wa dunia na mapenzi yake kwa Madrid yanajulikana”.
“Nimesikiliza maoni aliyosema Ronaldo na kama ninavyomjua, kamwe haiulizi klabu. Uhusiano wangu na yeye uko kamili, hakuna tatizo lolote. Cristiano ndiye mchezaji bora wa dunia, hilo liko wazi”
RONALDO ALISEMA NINI?
‘Kama ningekuwa madarakani, labda ningekuwa nimefanya mambo tofauti,’ Ronaldo alisema kuhusu usajili wa majira ya kiangazi wa Real Madrid.
“Nimekuwepo hapa tangu mwaka 2000″, Perez aliendelea.”Tangu hapo wachezaji wengi wamekuja na kuondoka na uzoefu wangu unaniambia kwamba wachezaji wengi wanaoondoka wanakuwa bora zaidi na wanaokuja wanazua maswali”
“Usajili wangu wa kwanza ulikuwa (Zinedine) Zidane na wa mwisho (kabla ya dirisha la majira ya kiangazi) alikuwa (Gareth) Bale. Na tulitoa ofa nzuri kwa Di Maria na alikataa”.