s4
Emmanuel Okwi akishangilia goli lake la kwanza msimu huu  akiichezea Simba sc
Na Baraka Mbolembole
Danny Mrwanda alifunga bao la kusawazisha mwanzoni mwa kipindi cha pili na kuisaidia timu yake ya Polisi Morogoro kupata sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Simba SC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Patrick Phiri aliwapanga wachezaji wanne wapya katika kikosi cha kwanza, golikipa, Hussein Shariff alianza katika nafasi ya majeruhi, Ivo Mapunda, nahodha wa zamani wa kikosi hicho,  Masoud Nassor ‘Chollo’ alipangwa nafasi ya ulinzi wa kulia huku, Jonas Mkude akianza kwa mara ya kwanza msimu huu akicheza sambamba na Pierre Kwizera na Shaaban Kisiga katika nafasi ya kiungo.
 Amis Tambwe, Emmanuel Okwi na Ramadhani Singano walianza katika safu ya mashambulizi na Simba ilionekana kucheza kwa kujiamini na kutawala mchezo katika dakika 45 za kipindi cha kwanza.
 Mkude hakupoteza pasi yoyote kati ya alizopiga katika nusu ya kwanza ya mchezo, aliichezesha timu yake kwa pasi fupi na ndefu zilizofika kwa walengwa.
 Phiri alionekamna kuvuka nje ya eneo lake na kupiga teke chupa ya maji iliyokuwepo pembeni yake baada ya kiki ya mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na mshambulizi Emmanuel Okwi dakika za mwisho kutokuwa na mafanikio.
Ilikuwa ni presha ambayo pengine ilikuwa ikiambatana na maswali ya kwanini…. Bao la kuongoza lililofungwa na Okwi katika dakika ya 32 liliambatana na mchezo wa ufundi, walinzi wa pembeni walipanda na kuwa viungo wazuri kiasi cha kuongoza namba katika eneo la katikati ya uwanja.
Kocha wa Polisi Moro, Adolph Richard aliwapanga viungo watatu wa katikati ya uwanja. Said Mkangu, James Ambrose na Nicolaus Kabipe walizidiwa kwa muda mwingi wa kipindi cha kwanza lakini Kisiga, Kwizera na Mkude walishindwa kutengeneza nafasi za kufunga mabao kiasi cha kufanya kusiwepo na shuti lolote lililopigwa golini.
Simba itacheza na Stand United katika mchezo wa tatu  huku timu hiyo ikiwa na wachezaji wengi wenye majeraha .
Phiri alimuanzisha Mohammed Hussein katika nafasi ya ulinzi wa kushoto na kijana huyo aliweza kutengeneza bao pekee la Simba alipopanda na kumpasia Okwi. Mwalimu, Adolph alimuingiza uwanjani nahodha wa timu yake, Nahoda Bakari mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kabipe.
 Polisi ilianza kujiamini na kupeleka mashambulizi langoni mwa Simba. Salum Machaku, Edgar Charles na Mrwanda walicheza kwa maelewano makubwa na Edgar alimtengenezea nafasi Mrwanda ambaye aliuwahi mpira uliowekwa ‘ njiani’ na kumzidi mbio nahodha wa Simba, Joseph Owino kisha kufunga bao safi la kusawazisha kisha kukimbia pembeni ya uwanja katika kona na kushangilia kwa ‘ staili ya kizee-zee’ kama afanyavyo mshambulizi, Mcameroon, Samuel Eto’o.
Simba ilisukumwa nyuma katika kipindi cha pili na mpira ambao ulipigwa na Edward Christopher ulizaniwa umezaa bao la pili kwa timu ya Polisi lakini marudio ya video yalionyesha kuwa mpira huo uligonga ‘ mwamba wa juu’ na kutua juu ya mstari haukuwa umeingia golini.
 Phiri alifanikiwa katika kipindi cha kwanza wakati timu yake ilipokuwa na pumzi, lakini safu ya kiungo haikufanya kazi nzuri ya kutengeneza nafasi licha ya kumiliki mpira kwa muda mrefu.
Jaribio pekee la hatari la Polisi katika kipindi cha kwanza ni lile lililofanywa na mlinzi wa pembeni Hassan Maganga ambaye alipiga mpira wa adhabu ndogo lakini Shariff aliucheza vizuri.
Kipindi cha pili kilikuwa kigumu kwa Simba, Nahoda alipiga pasi za kwenda mbele huku akiichezesha timu yake, Machaku akawa anakimbia na mpira pembeni ya uwanja huku Danny akivuruga  utulivu wa Owino na Hassan Isihaka kwa mbio zake za mara kwa mara. Mabadiliko ya kwanza ya Phiri ni yale ya kumtoa Cholo na kumuingiza uwanjani kijana William Lucian dakika ya 56.
 Alilenga kupunguza mashambulizi ya Polisi ambao walitambua uchovu aliokuwa nao Cholo. Lucian aliziba vizuri nafasi hiyo licha ya Polisi kumuingiza uwanjani kiungo, Suleiman Kassim dakika nane baada ya kumthibiti, Machaku.
Elius Maguli aliingia mahala kwa Tambwe zikiwa zimesalia dakika 16 mchezo kumalizika, Simba ilionekana kuchoka na Phiri alihitaji nguvu mpya kwa ajili ya kufuata mipira katikati ya uwanja na kuipeleka mbele.
 Tambwe hakuonekana kwa sababu hakuna nafasi iliyotengenezwa, Maguli aliingia kuimarisha kiungo ama safu ya mashambulizi? Simba inakwenda vibaya mwanzoni mwa msimu. Timu hiyo inaonekana kutokuwa na pumzi kiasi cha kupoteza umakini wanapoanza kuchoka.
Ulimuona Lulanga Mapunda? Katika umri wa miaka 31 sasa anawafundisha vijana namna beki tano anavyotakiwa kuwa. Anacheza kwa utulivu, ana wapanga wenzake na kuwatuma sehemu zenye mapengo, ni mchezaji anayeusoma mpira vile unavyokwenda na kujipanga vizuri. Huyu alistahili kuwa mchezaji bora wa mchezo wa huu.

 
Top