WEKUNDU wa Msimbazi, Simba sc, wamelala bao 1-0 dhidi ya wakusanyaji mapato wa Uganda, klabu ya URA katika mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyomalizika dakika chache zilizopita uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Kipigo hiki ni cha kwanza kwa kocha Patrick Phiri tangu arudi kuifundisha klabu hiyo kwa mara ya tatu akirithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic aliyetimuliwa kazi mwezi wa nane baada ya Tamasha la ‘Simba Day’, Agosti 9 mwaka huu.
Baada ya mechi ya leo, kesho asubuhi, kikosi kizima cha Simba kinapanda ndege kuelekea mkoani Mtwara ambapo kitacheza mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji, Ndanda fc.
Wikiendi iliyopita, Simba chini ya Phiri walicheza mechi ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya mabingwa watetezi wa Kenya, Gor Mahia na kushinda mabao 3-0.
Licha ya kushinda, vijana hao wa Msimbazi walionesha kandanda safi hususani kipindi cha pili, lakini leo wameshindwa kufurukuta mbele ya timu ngumu ya URA.
URA walionekana kuzuia mianya ya washambuliaji wa Simba waliokuwa na hamu ya kupata mabao akiwemo Emmanuel Okwi, Pual Kiongera na wengineo.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba sc, Said Tully amekiri kuwa URA walikuwa wazuri zaidi ya Simba na wanatamani kuona kikosi hao kinaimarika kama vijana hao wa Uganda.
Tully amesema kikosi cha Simba kilijitahidi kupambana, lakini ngome ya URA ilikuwa ngumu kuipenya.
Goli la URA lilitokana na mabeki wa Simba kuzubaa kuokoa mpira wa krosi uliopigwa langoni mwao.
Uchambuzi wa mechi hiyo utakujia hapa hapa…stay tuned!