Mapinduzi ya mashetani: Louis van Gaal (katikati) akijiandaa kumtambulisha wachezaji wake wa mwisho katika usajili wa majira ya kiangazi, Radamel Falcao (kushoto) na Daley Blind (kulia) katika dimba la Old Trafford
RADAMEL Falcao amesema Manchester United watakapomsaini kwa mkataba wa muda mrefu baada ya kumaliza wa sasa wa paundi milioni sita kwa mkopo, anataka kukaa klabuni hapo kwa miaka mingi na kuweka historia Old Trafford.
Mshambuliaji huyo wa Colombia alitambulishwa sambamba na kiungo aliyesajiliwa kwa paundi milioni 14, Daley Blind jana alhamisi baada ya kufanya mazoezi kwa mara ya kwanza chini ya Louis van Gaal.
United wana chaguo la kumnunua Falcao kutoka Manaco majira yajayo ya kiangazi kwa dau la paundi milioni 52 na wamekubali kumlipa mshahara wa paundi lakini 2 na elfu 80 msimu huu.
Akizungumza kwa kuchanganya Kiingereza na Kihispania, Falcao alisema: “Nina matumaini ya kukaa Manchester United kwa miaka mingi na kutengeneza historia. Nilipokuwa FC Porto na Atletico Madrid siku zote nilikuwa napenda kujiimarisha na niliota kucheza timu kama hii. Sasa nataka kukaa hapa kwa miaka mingi”.