Na Baraka Mbolembole
Akiwa na uzoefu wa kufanya kazi katika shule ya kukuza na kuendeleza vipaji ya klabu mashuhuri nchini, England, Birmingham City, Stewart John Hall alitua Azam FC kuchukua nafasi ya Itamor Amourin na akafanya kazi kuanzia Januari, 2011 hadi, Agosti, 2012 alipoondoka na kwenda kujiunga na Sofa Paka ya Kenya. Baada ya kuiongoza timu hiyo kufika fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ambayo Azam ilipata nafasi hiyo kwa mara ya kwanza kufuatia kumaliza katika nafasi ya pili ya ligi kuu Bara, msimu wa 2011/12.
Hall alirejea kwa mara ya pili baada ya miezi mitatu kufuati maombi mengi kutoka kwa wachezaji wa Azam ambao walikiri wazi kutoelewa mbinu za Mwalimu raia wa India, Boris Bunjak ambaye alichukua nafasi ya ukocha mara baada ya kuondoka kwa Hall, mwezi, Agosti. Hall alirejea kwa mara ya pili Azam mwezi Novemba na kumalizia michezo miwili ya mzunguko wa kwanza msimu huo. Kwa mara nyingine akaisaidia Azam kumaliza katika nafasi ya pili hivyo kupata nafasi kwa mara nyingine kuiwakilisha nchi katika michuano ya vilabu barani Afrika.
Katika michuano ya pili ya Kimataifa kwa timu hiyo baada ya ile ya Kagame Cup, Hall aliweza kuisaidia Azam kufika hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la shirikisho wakishinda michezo mitano kati ya sita mwaka 2013. Stewart alishiriki kikamilifu kuiandaa AZam kwa kufanya usajili makini ambao uliongezea baadhi ya nafasi chache. Aliamua kuwatumia wachezaji vijana kama mkakati wa kuifanya timu kuwa na uwanja mpana wa kuchagua wachezaji. Mafanikio ya Azam yametokana na maandalizi, mikakati na mawazo ya Stewart licha ya kuondoka mara baada ya kumalizika kwa michezo ya mzunguko wa kwanza msimu uliopita.
Hall alikuwa mwalimu wa nne wa Azam katika kipindi cha miaka miwili na nusu, na alikuwa mwalimu wa tatu wa kigeni. Awali, Azam FC ilikuwa chini ya makocha, Habib Kondo na aliyekuwa msaidizi wake, Mohammed Seif wakati walipopambana na kupanda ligi kuu, mwaka, 2008. Baada ya timu hiyo kupanda ligi kuu uongozi wa juu ukamleta mwalimu, Mbrazil, Neidor Dos Santos na msaidizi wake, Itamor Amourin na kumpatia majukumu ya usomaji wa mchezo, Mohammed kama lengo la kuifanya klabu hiyo kuwa washindani katika ligi kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2008/09.
Santos alifukuzwa kazi mwezi, Machi, 2009 baada ya timu hiyo kuwa hatarini kushuka daraja. Itamor akakaamu nafasi ya ukocha mkuu hadi mwishoni mwa msimu huku akisaidia timu hiyo kusalia katika ligi kuu baada ya ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya waliokuwa mabingwa, Yanga SC siku ya mwisho wa msimu. Hakika msimu wa kwanza wa timu hiyo ulikuwa mgumu na pengine uamuzi wa kumuachisha kazi, Santos ungechelewa kwa wiki moja zaidi, Azam FC ingeshuka daraja. Itamor alifanya usajili mpya kwa ajili ya msimu wa 2009/10.
Licha ya klabu kuwa na mtazamo wa kutumia wachezaji vijana, Itamor alishuhudia wachezaji kama, Jamal Mnyatte, Sino Agustino, Salum Machaku wakiondoka ili kuwapisha wachezaji wa kigeni ambao walisajiliwa kwa wingi kwa kufuata historia zao za miaka ya nyuma na si viwango vyao vya uchezaji.
Inasemekana wachezaji wengi walisajiliwa nje ya mapendekezo ya Mbrazil huyo ambaye alipendekeza kuachwa kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi, walioshuka viwango na wale waliokuwa na matatizo ya mara kwa mara ya kinidhamu. Shekhan Rashid, Said Sued, Shaaban Kisiga ni baadhi ya wachezaji ambao waliondoka kwa sababu tofauti mara baada ya kumalizika kwa msimu. Itamor aliisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Simba SC waliokuwa mabingwa na Yanga waliomaliza katika nafasi ya pili.
Hall alikuwa aliwasili kwa mara ya kwanza Tanzania, septemba, 2009 kama mkurugenzi wa ufundi wa timu ya Taifa ya Tanzania. Alikuwa na mwaka mmoja wa mafanikio akiwa kocha mkuu wa Zanzibar Heroes nawakati Azam FC walipohitaji kocha mbadala wa Itamor mara baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza msimu wa 2010/11, takwimu nzuri za Stewart na kiwango chake cha ufundishaji kilifanya haraka Azam kumpatia mkataba wa miaka miwili na nusu mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Challenge Cup, Disemba, 2010.
Azam ambayo ilikuwa imefanya usajili mkubwa katikati ya mwaka 2010 walipowasaini wachezaji mahiri kama, Ramadhani Chombo, Jabir Aziz, Mrisho Ngassa, Osborne Monday, Crispian Odulla, Dan Wagaruka, Patrick Mafisango na wengineo wengi ilianza mzunguko wa pili chini ya Hall kwa kiwango cha juu huku wakicheza pasi za haraka na mchezo wa kasi dhidi ya Simba katika ushindi wa mabao 3-1. Azam iliongoza ligi kwa muda mrefu na ilionekana kama ingetwaa ubingwa wake wa kwanza wa Tanzania Bara katika msimu wake wa tatu wa ligi kuu. Iliishia katika nafasi tatu kwa mara ya pili mfululizo lakini tayari timu ilikuwa imeingia katika orodha ya timu tishio katika ligi kuu.
Hall akasimamia usajili kwa ajili ya msimu wa 2011/12. Aliamua kuwatumia wachezaji wengi zaidi wa Kitanzania katika msimu huo na kuachana na wachezaji wengi wa kigeni. Azam ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Simba waliotwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi sita. Yalikuwa ni mafanikio makubwa kwa timu hiyo kwani iliweza kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa. Licha ya kuukosa ubingwa baada ya kuongoza ligi hadi mechi nne kabla ya msimu kumalizika, Hall alifanikiwa katika mtazamo wa wowote ule. Azam ilimaliza juu ya Yanga katika msimu huo na ilifanikiwa kuwafunga mabingwa hao mara 24 wa kihistori katika michezo yote miwili hivyo kudhihirisha kuwa wameimarika katika suala la ufundi na kujituma.