Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Yanga ina kikosi kilichojaa wachezaji, ila kuwakosa baadhi ya wachezaji muhimu inaweza kuwa pigo kwa timu hiyo kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii, Jumapili hii dhidi ya Azam FC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha wa timu hiyo ameanza kukabiliwa na majeruhi katika kikosi chake, kiungo mshambulizi, Andrey Coutinho aliumia sehemu ya enka yake ‘ kifundo cha mguu’ siku ya Jumatano wakati timu yake ilipolazimishwa suluhu-tasa na Polisi Dar es Salaam katika mchezo wa kirafiki.
Mchezo huo ulifanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola. Coutinho alikanyaga shimo lililokuwepo uwanjani hapo wakati akikokota mpira. Yanga imekuwa ikiutumia uwanja huo kwa mazoezi yake ya kila siku kwa kuwa hawana uwanja wao binafsi.
Uwanja huo si mzuri kwani una mashimo, nyasi zipo chache na za hovyo, ni mgumu kwa kiasi hivyo unaweza kuwa hatari zaidi kwa wachezaji. Maximo yupo katika wakati mgumu kwa kuwa si Coutinho peke yake, nahodha, Nadir Haroub anasumbuliwa na misuli ya paja.
Ikumbukwe kiungo Frank Domayo alipata matatizo sugu kama hayo akiwa na Yanga kabla ya kusajiliwa na Azam msimu huu. Yanga wanatakiwa kutafuta uwanja mzuri wa kufanyia mazoezi ambao hautakuwa sababu ya kuwapoteza wachezaji wao muhimu.
Uwanja mgumu unafanya wachezaji kupata matatizo ya enka, huku mwalimu akipata wakati mgumu kuwekeza mbinu zake za ufundi.