Wakati Kocha wa Tanzania Prisons, David Mwamwaja ameelekeza nguvu zote katika mechi inayofuata ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba, mashabiki wa soka jijini Mbeya wamesema mwaka huu ni
wa tabu kwa mkoa wao kisoka.
Baada ya Prisons kukubali kichapo cha magoli 2-1 dhidi ya JKT kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini hapa jana huku Mbeya City ikilala 1-0 dhidi ya Azam FC Jumamosi, kauli iliyotawala mitaa mbalimbali ya mji huu ni ‘mwaka wa tabu Mbeya’.
Magoli ya Najim Magulu dakika ya 27 na Jabir Aziz aliyefunga kwa penalti dakika ya 51 yaliipa ushindi wa kwanza msimu huu JKT Ruvu inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Felix Minziro.
Akizungumza na mtandao huu mjini hapa jana, Mwamwaja alisema kikosi chake kilirejea kambini juzi kuanza maandalizi ya mechi yao dhidi ya Simba ambayo alidai itakuwa ngumu kwa kuwa Simba watakuwa wanasaka
ushindi wa kwanza msimu huu.
“Kikosi changu cha ni kizuri kuzidi cha msimu uliopita, mechi ya jana (juzi) tuliponzwa na kipa (Beno Kakolanya). Magoli yote yametokana na makosa yake, tumeshaanza kurekebisha kasoro hiyo, kufikia Jumamosi tunaamini atakuwa sawa,” alisema Mwamwaja.
“Mechi yetu ya Jumamosi itakuwa ngumu, pengine kuzidi mechi zote nne tulizocheza msimu huu hadi sasa. Ninatambua Simba wataingia uwanjani kusaka ushindi wao wa kwanza msimu huu baada ya kuambulia sare katika mechi zote walizocheza, lakini hata sisi tunahitaji ushindi ili tujiweke pazuri na kulinda heshima ya uwanja wetu wa nyumbani,”
alisema zaidi kocha huyo wa zamani wa Simba.
 
Top