Simba SC imepata ‘ nafuu’ baada ya golikipa wake namba moja, Ivo Mapunda kuanza mazoezi siku ya jana nchini, Afrika Kusini. Ivo aliumia kidole wiki tatu zilizopita, alikosa michezo miwili iliyopita dhidi ya Polisi Morogoro na Stand United na nafasi ya kipa namba moja ikaangukia kwa Hussein Shariff. Mapunda ni golikipa mzoefu na amewahi kushiriki mara nyingi katika mipambano ya mahasimu wa soka la Tanzania.
Ni faraja kwa mashabiki wa timu yake kwa sababu watakuwa wageni wa Yanga SC siku ya Jumapili katika mchezo wa ligi kuu. Shariff alicheza michezo dhidi ya Polisi Moro na Stand alionyesha ‘ wasi wasi’ wakati alipopewa nafasi ya kuichezea Simba kwa mara ya kwanza, lakini golikipa huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Vijana na klabu ya Mtibwa Sugar anaweza kucheza vizuri zaidi ya Mapunda ambaye takribani wiki mbili amekuwa akiuguza majeraha ya kuvunjika kidole.
hussein-sharrif-Casillas-546x2911
Mwalimu, Patrick Phiri anaweza kumuanzisha, Ivo kutokana na uzoefu wake lakini ikumbukwe kuwa Shariff anaweza kucheza vizuri endapo atajiamini na anaweza kuibuka mchezaji bora wa mechi kama ataaminiwa. Shariff yuko ‘ fiti’ kuliko, Ivo lakini mara zote walimu hupendelea kuwatumia wachezaji wazoefu wenye ubora katika michezo mikubwa. Je, Ivo yupo katika ubora unaofaa kupangwa katika kikosi cha kwanza siku ya Jumapili?
Kiwango kibovu msimu huu kimefanya kuwepo mambo mengi yasiyofurahisha. Hakuna mjadala kuhusu kipaji cha Ivo kipa ambaye anaweza kuitoa timu katika presha ya kushambuliwa na kujifanya ‘ kuumia’ ili wenzake wapumzike. Kumpanga Ivo dhidi ya Yanga akiwa na mazoezi ya siku nne au tatu inaweza kuwa ‘ Kamari kubwa’,
Kuna ubaya na kuna uzuri wake. Ubaya ni pale timu itakapokuwa katika presha, Yanga watamchosha mapema Ivo, lakini ikiwa ni Shariff mchezaji huyo anaweza kuanza vibaya lakini akamaliza mechi akiwa ‘ shujaa’ kwa kuwa anapojiamini anaweza kucheza vizuri akilinda lango lake huku akiwapanga na kuwaongoza wachezaji wenzake wa safu ya ulinzi. Lipi chaguo bora kati ya Ivo Mapunda na Hussein Shariff katika lango la Simba wakati wa mchezo dhidi ya Yanga?.
 
Top