Kwa sasa ligi kuu ina timu 14 pekee, ambazo zinashiriki na kila msimu zilikuwa zikishuka timu tatu pekee na kupanda tatu kutoka daraja la kwanza
TIMU nne zinatarajiwa kupanda Ligi Kuu Tanzani Bara msimu ujao huku timu mbili pekee msimu huu zikishuka daraja ili kuweza kuandaa mpango mpya wa msimu wa mwaka 2015/2016, ambapo timu 16 ndizo zitakazoshiriki ligi hiyo.
Kwa sasa ligi kuu ina timu 14 pekee, ambazo zinashiriki na kila msimu zilikuwa zikishuka timu tatu pekee na kupanda tatu kutoka daraja la kwanza.
Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga, ameiambia Goal, kuwa msimu ujao ni timu nne kutoka daraja la kwanza ndizo zitakazopanda na mbili zitashuka katika ligi ya msimu huu.
Mwakibinga amesema mpango huo utaanza msimu ujao na kwa sasa timu zilizopo daraja la kwanza wanatakiwa kuonyesha bidii kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanafanikiwa kupanda.
“Tumedhamiria kuzidi kuiboresha ligi yetu tumekuwa tukipata lawama sana kuhusu uchache wa timu na idadi ndogo ya mechi ambazo zimekuwa haziwasaidii sana wachezaji wetu ambao wamekuwa wakicheza mechi chahe tofauti na ligi zenye timu 18 au 20,”amesema Mwakibinga.
 
Top