Miamba ya England, timu za Manchester United na Chelsea zitapambana katika mchezo wa raundi ya tisa katika ligi kuu ya England siku ya Jumapili hii katika uwanja wa Old Trafford. Chelsea inakwenda Manchester kucheza na ‘ Mashetani Wekundu’ ikisaka rekodi ya kucheza michezo sita pasipo kupoteza dhidi ya wapinzani wao ambao wanapambana kujiweka sawa tangu alipoondoka, Sir Alex Ferguson.
Mshambulizi, Mcameroon, Samuel Eto’o alikuwa ‘ shujaa’ katika mchezo wa mwisho wa timu hizo zilipokutana katika uwanja wa Stamford Bridge msimu uliopita. Chelsea ilishinda kwa mabao 3-1, Mwezi Januari, Eto’o alifunga mabso yote katika muda wa dakika 49, wakati bao pekee la United lilifungwa na mshambulizi, Javier Hernendez ambaye kwa sasa anaichezea Real Madrid kwa mkopo wa muda mrefu.
Chelsea haijafungwa na United katika michezo mitano iliyopita, mara ya mwisho kushinda katika uwanja wa Old Trafford ilikuwa ni May, 2013 waliposhinda kwa bao 1-0. Bao hilo lilifungwa na Juan Mata katika dakika ya 87 liliwahakikishia Chelsea nafasi ya kufuzu kwa ligi ya mabingwa. Chelsea haijapoteza mchezo dhidi ya United katika safari tano ilizokwenda, Old Trafford na inaweza kurudia yale ya miaka ya 2003-05 walipocheza miaka yote hiyo bila kufungwa na United katika uwanja huo.
Ti,u hizo hazikufungana katika mchezo wa kwanza msimu uliopita katika uwanja wa Stamford Bridge wakati huo David Moyes alipokuwa kocha wa United. Chini ya Luis Van Gaal , United imedhamiria kufanya vizuri msimu huu huku kocha huyo raia wa Uholanzi akisema kuwa kikosi chake kinaweza kutwaa ubingwa msimu huu licha ya watu wengi kukibeza.
United ililazimika kupambana mno ili kuswazisha katika mchezo dhidi ya West Brom.Kiungo-mlinzi, Daley Blind alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 87. United ilishtushwa na bao la kiungo, Stephen Sessegnon katika dakika ya nane. Kiungo Maruoane Fellaini alisawazisha bao hilo katika dakika ya 48 dakika tatu tangu alipoingia uwanjani kuchukua nafasi ya Ander Herrera. United haijapata ushindi katika mchezo wowote wa ugenini msimu huu lakini wamekuwa wakifanya vizuri katika uwanja wa nyumbani.
Chelsea imekuwa na mwanzo mzuri msimu huu, walishinda kwa mabao 2-1 dhidi ya timu ngumu ya Crystal Palace wiki iliyopita lakini ilimpoteza mchezaji wake wa nafasi ya ulinzi, Cesar Azpilicueta ambaye alionyeshwa kadi nyekundu. Chelsea iliifunga Arsenal kwa mabao 2-0 wiki mbili zilizopita, na ilizimishwa sare na Manchester City katika uwanja wa Etihad wiki tatu nyuma hivyo timu hiyo itakwenda Old Trafford ‘ ikijiamini’ licha ya kuwa na wasiwasi wa wachezaji wao Diego Costa na Loic Remy kucheza mchezo huo.
Washambuaji hao chaguo la kwanza na la pili waliumia kwa nyakati tofauti, Costa akiwa na mabao nane msimu huu aliukosa mchezo wa ligi ya mabingwa Ulaya dhidi Maribor katikati ya wiki hii, lakini mchezaji huyo tayari ametoka katika meza ya matibabu na anaweza kucheza. Remy alifunga bao la kwanza katika ushindi wa mabao 6-0 wa Chelsea dhidi ya Maribor lakini aliumia dakika chache baadae wakati akishangilia bao hilo, habari za awali zilisema kuwa mshambulizi huyo wa Ufaransa atakuwa nje ya uwanja kwa wiki mbili.
Jose Mourinho alisema kuwa hakuna mchezaji yeyote kati ya Costa na Remy atakayecheza mchezo dhidi ya United lakini kuna uwezekano wote wakacheza. Eden Hazard alimuachia mkwaju wa penalti, Didier Drogba katika mchezo dhidi ya Maribor ili kumfanya mshambulizi huyo kujiamini kuelekea mchezo dhidi ya United. Drogba alifunga bao lake la kwanza kwa Chelsea baada ya kurejea msimu huu anaweza kuanza sambamba na Hazard na Oscar katika safu ya mashambulizi ya Chelsea.
Michael Carrick alikuwa katika benchi siku ya Jumatatu, kiungo huto hajacheza mchezo wowote msimu huu baada ya kuwa katika majeraha ya muda mrefu, urejeo wa Carrick unaweza kuimarisha sehemu ya ulinzi na kiungo ya timu hiyo ambayo imekuwa ikipwaya sana. Blind amekuwa akicheza kama kiungo wa ulinzi, nyuma yake wakicheza walinzi, Marcos Rojo na Phill Jones. Van Gaal anaweza kunufaika na Carriuck kwa kuwa mchezaji huyo anakaba kwa kuziba nafasi na Chelsea ni timu inayopitisha mipira katika ‘ njia’, Carrick atafaa kucheza na viungo wenye ubunifu wa Chelsea.
Cecs Fabregas, Willian na Nemanja Matic wataanza katika nafasi ya kiungo wa Chelsea. United inataraji ,kuwaanzisha washambuliaji wake mahiri , nahodha, Wayne Rooney, Robbin Van Persie na Angel Di Maria. Blind, Mata, wanaedza kuanza moja kwa moja katika nafasi ya kiungo huku Van Gaal akitafakari ni nani hasa wa kuungana nao kati ya Fellaini, Carrick. Kama United itacheza kwa nguvu kama walivyocheza dhidi ya Everton wiki mbili zilizopita watakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Chelsea itakuwa na nafasi ya kushinda lakini si ya moja kwa moja kwa kuwa baadhi ya wachezaji wake muhimu ni majeruhi, hawapo fiti. Nahodha, John Terry, Garry Cahil watacheza katika ngome ya kati, huku Banslav Ivanovic na Fillipe Luiz watacheza sehemu za ulinzi wa pembeni ambazo kwa upande wa United watacheza, Rafaer da Silva na Luke Shaw. Nani mshindi wa mechi hii? Tusubiri na tuone, ila kubashiri unaruhusiwa……