Kikosi cha kocha Mbrazil Marcio Maximo kimeendelea na mazoezi leo asubuhi katika Uwanja wa Boko Veterani kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom siku ya jumamosi dhidi ya timu ya Simba SC, kipute kitakachofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo iliingia kambini Hoteli ya Landmark kujiandaa na mechi hiyo, imekua ikifanya mazoezi asubuhi na jioni katika uwanja wa Boko na wakati mwingine kwenye ufukwe wa bahari ya Hindi eneo la Bahari beach kuhakikisha wachezaji wanakua fit kwa ajili ya mchezo huo.
Kocha Marcio Maximo amesema anashukuru vijana wake wote wanaendelea vizuri, wanaonekana kuyashika vilivyo mafunzo yake, umakini umeongezeka, na morali ni ya hali ya juu kuelekea kuzisaka pointi 3 siku ya jumamosi.
Akiongelea mchezo wenyewe wa jumamosi dhidi ya watani wa jadi Simba SC, Maximo amesema anatambua michezo inayokutanisha watani huwa haitabiriki, na mara yingi matokeo yake huwa ni ya kushangaza, ila ana uzoefu na michezo hiyo na kusema atajitahidi kuhakikisha timu yake inapata ushindi.
Naitambua Simba SC ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri na wengi wao niliwahi kuwafundisha wakati nilipokua kocha mkuu wa timu ya Taifa, hivyo najua nitatumia mfumo upi ambao utanisaidia kupata ushindi.
Aidha kocha Maximo amewaomba wapenzi wa Young Africans kujitokeza kwa wingi uwanjani siku ya jumamosi kuwapa sapoti vijana na kuonyesha Yanga ni timu ya watu kwa kuujaza uwanja wote na kuwashangilia wachezaji, kuonyesha kuwa ni kitu kimoja na wachezaji nao hawatawangusha watawapa furaha baada ya dakika 90 za mchezo.
Katika kikosi kilichoingia kambini kujiandaa na mchezo huo wa jumamosi, ni wachezaji watatu tu ndio majeruhi Kelvin Yondani (nyonga), Geilson Santana"Jaja" (enka) na Nadir Haroub "Cannavaro" ambaye aliumia katika timu ya Taifa, hawakuweza kufanya mazoezi jana na leo asubuhi na wenzao kutokana na kuendelea na matibabu chini ya usimamizi wa karibu wa daktari wa timu Dr Suphian Juma.