UNAJUA kwamba Ruvu Shooting ndiyo timu ya mwisho kufungwa na Simba katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) katika miezi nane iliyopita? TEGA SIKIO…
Mara ya mwisho Simba kuibuka na ushindi VPL ni pale ilipoifunga Ruvu Shooting mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam msimu uliopita, ndipo bundi akaingia na kuanza kuitafuna klabu hiyo uwanjani hadi leo.
Ikumbukwe kuwa Simba iliyolazimika kuwatimua makocha wake Abdallah ‘King’ Kibadeni na msaidizi wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ mara tu baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa VPL msimu uliopita, kikosi kikiwa nafasi ya nne nyuma ya Yanga, Azam na Mbeya City, Simba ilishinda mechi tatu tu mzunguko wa pili ikiwa chini ya waajiriwa wapya, Mcroatia Zdravko Logarusic na msaidizi wake Selweman Matola.
Simba ilizishinda Rhino Rangers, JKT Oljoro iliyoshuka daraja na Ruvu Shooting ya kocha Mkenya Tom Alex Olaba.
Baada ya hapo Simba ilifungwa na Mgambo Shooting, Azam FC, JKT Ruvu, Ashanti United iliyoshuka daraja na Coastal Union huku ikitoka sare na Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Mbeya City, Tanzania Prisons na Yanga.
Msimu huu Simba imecheza mechi sita za VPL, zote ikiambulia sare, 2-2 nyumbani dhidi ya Coastal Union, Polisi Morogoro, Stand United na suluhu dhidi ya Yanga kabla ya 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons na 1-1 vinara wa msimamo Mtibwa Sugar.
                                                 
Simba vs Ruvu Shooting msimu uliopita
Kwa kifupi, Simba imecheza mechi 12 za VPL bila ushindi baada ya kuwafunga 3-2 ‘maafande’ wa Ruvu Shooting miezi nane iliyopita. Je, itaanza kupata ushindi dhidi ya timu hiyo ya Pwani Jumapili na kuondoa gundu la sare?
Tayari uongozi wa Ruvu Shooting kupitia kwa msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire umewweka wazi kuwa hauko tayari kuona timu yake inatumika kumaliza gundu hilo linaloukabili uongozi wa Simba chini ya Rais wake, Evans Aveva ambaye sera yake ya pointi 3 magoli 3 inaonekana kufeli.
“Tumesikia wamempa kocha wao (Mzambia Patrick Phiri) mechi mbili ikiwamo yetu kwamba lazima ashinde vinginevyo wanamtimua. Tunachoweza kumshauri Phiri ni kwamba akate tiketi mapema na kutanguliza mabegi na vifaa vyake uwanja wa ndege maana sharti hilo ni gumu mno mbele ya Ruvu Shooting,” anasema Bwire.
Lakini, Aveva amekaririwa leo na magazeti makubwa nchini akieleza kuwa wametengua sharti lao kwa benchi la ufundi baada ya kubaini kuna matatizo mengine ndani ya timu yao.
Simba baada ya kuambulia sare sita mfululizo msimu huu, tayari inaonekana kuvurugana baada ya kuwasimamisha viungo wake Amri Kiemba na Shaban Kisiga pamoja na winga Haroun Chanongo kwa madai ya utovu wa nidhamu na kucheza chini ya kiwango.
SONY DSC
Timu hiyo ya msimbazi inakutana na kikosi cha kocha Olaba, Ruvu Shooting ambacho kimepoteza ugenini 1-0 mechi yake iliyopita dhidi ya mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumamosi.
Ruvu Shooting pia imeuanza vibaya baada ya kupoteza mechi zake mbili za mwanzo 2-0 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons na 2-0 ugenini dhidi ya Azam FC kabla ya kutoka suluhu nyumbani dhidi ya Mbeya City, ikashinda 3-1 ugenini dhidi ya Ndanda FC, ikashinda 1-0 nyumbani dhidi ya Polisi Morogoro kabla ya kupoteza Jumamosi.
Timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Kitengo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), inakamata nafasi ya saba ikiwa na pointi saba. Imefunga magoli manne huku ikiruhusu nyavu zake kutikishwa mara sita wakati Simba iko nafasi ya tisa ikiwa na pointi sita, imefunga magoli sita na kufungwa sita pia.
Mechi nyingine za mwishoni mwa wiki zitawakutanisha vinara wa msimamo, Mtibwa Sugar dhidi ya ‘ndugu zao’ Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani km 100 kutoka mjini Morogoro, Stand United wataialika timu iliyo mkiani baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo, Mbeya City kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga wakati JKT Ruvu iliyofunga 2-1 na Polisi Morogoro Jumamosi, itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC kwenye Uwanja wa Azam.
Yanga watakuwa waliorejea baada ya kupigwa 1-0 na Kagera Sugar wakiwa Kanda ya Ziwa, watawakaribisha Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi, Tanzania Prisons watakuwa wageni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati mabingwa watetezi Azam FC, baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu (nyumbani) na Ndanda FC (ugenini), watakuwa wenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wao wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam Jumamosi.
 
Top