Ligi kuu ya soka Tanzania Bara imesimama kupisha michezo ya kimataifa ambayo itapigwa dunia nzima kuanzia mwishini mwa wiki hii. Hadi sasa kila timu imeshuka dimbani mara saba. Vinara wa ligi hiyo Mtibwa Sugar, mabingwa watetezi, Azam FC na Yanga SC ndiyo timu zilizoshinda michezo mingi, timu hizo zilizo katika nafasi tatu za juu zote zimeshinda michezo minne.
Wakati, Azam na Yanga zikiwa tayari zimepoteza michezo miwili, Mtibwa na Simba SC ndiyo timu pekee ambazo hazijapoteza mchezo wowote hadi sasa. Mtibwa ikiwa na pointi 17 imetoa sare mara tatu wakati Simba imeshinda mara moja na kutoa sare mara tano. Simba ndiyo timu iliyotoa sare mara nyingi zaidi msimu huu kabla ya kupata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting mwishoni mwa wiki iliyopita.
Coastal Union walipokea kipigo cha pili msimu huu baada ya kufungwa na Azam mabao 2-1. Coastal ambayo ilikuwa timu iliyotoa sare mara nyingi zaidi msimu uliopita, ipo katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 11. Pointi nne nyuma ya Mtibwa, na pointi mbili nyuma ya Azam na Yanga. Mshambulizi raia wa Kenya, Rama Salim ameweza kufunga mabao manne hadi sasa akifungana na washambuliaji, Didier Kavumbagu ( Azam FC), Danny Mrwanda ( Polisi Morogoro), Rashid Mandawa ( Kagera Sigar) na Ame Ally ( Mtibwa) ambao wote wamefunga mabao manne.

Maajabu hadi sasa ni kufanya vibaya kwa timu ya Mbeya City. City imepoteza michezo minne msimu huu wameshinda mara moja tu huku wakitoa sare mara mbili. Kikosi hiko cha kocha mzawa, Juma Mwambusi kipo mwishoni kabisa mwa msimamo kikiwa na pointi tano. City imekosa makali licha ya safu ya ulinzi kuonesha ukakamavu. Ikiwa imemuongeza mshambulizi Themi Felix ‘ Mnyama’ kutoka timu ya Kagera Sugar, City imefanikiwa kufunga bao moja tu katika michezo saba huku wakiruhusu mabao manne katika michezo saba.
Msimu uliopita ambao ulikuwa ni wa kwanza kwa timu hiyo katika ligi kuu, City ilicheza pasipo kufungwa kwa muda mrefu hadi walipokuja kupoteza mbele ya Yanga, Mwezi Februari katika uwanja wa Taifa. Imefungwa na Mtibwa katika uwanja wa nyumbani msimu huu lakini bado Mwambusi anaweza kutumia usajili wa dirisha dogo kuimarisha timu hiyo iliyo nyuma kwa tofauti ya pointi kumi na vinara Mtibwa.
Ndanda FC ambayo inacheza ligi kuu kwa mara ya kwanza ndiyo timu iliyofungwa mabao mengi zaidi hadi sasa, timu hiyo iliyomtimua kocha wake Dennis Kitambi baada ya kucheza michezo minne tu imeruhusu mabao 12 huku wakifunga mabao tisa katika michezo sabailiyopita. Stand United ambayo iliifunga City kwa bao 1-0 siku ya Jumamosi iliyopita imeruhusu mabao tisa huku wakishinda michezo michezo miwili na kutoa sare mara tatu. Timu hiyo ya Shinyanga imepoteza michezo miwili tu, ina pointi tisa sawa na timu za Simba, Mgambo JKT, Polisi Morogoro.
                                         
Kagera Sugar chini ya Mganda, Jackson Mayanja ipo katika nafasi ya tano ikiwa na pointi kumi sambamba na JKT Ruvu. Kagera ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Mtibwa siku ya Jumapili ni imefunga mabao manne tu huku wakiruhusu mabao sita katika nyavu zao. Imeshinda mara mbili na kutoa sare mara nne, huku wakipoteza mchezo mmoja tu. Wakati Fred Minziro kocha wa JKT Ruvu akifurahia mwanzo mzuri msimu huu, timu hiyo ya Pwani imekusanya pointi kumi baada ya kushinda mara tatu na kutoa sare mara moja huku wakipoteza michezo mitatu. JKT Ruvu imefunga mabao tisa na kuruhusu mabao suta.
                  
City, Ndanda FC, na Tanzania Prisons zinakama nafasi tatu za chini katika msimamo. Ndanda na Prisons wamekusanya pointi sita katika michezo saba waliyocheza. David Mwamaja, kocha wa Prisons amesema kuwa watatumia mapumziko ya kusimama kwa ligi ili kurejesha hali iliyopotea kwa wachezaji wake. Prisons imecheza michezo sita mfululizo bila kupata ushindi baada ya kuishinda Ruvu Shooting siku ya ufunguzi. Imetoa sare mara tatu huku wakipoteza michezo mitatu. Imefungwa mabao nane huku wakifunga mabao sita,
 
Top