BAADA ya timu yake kushindwa ‘kufanya kweli’ msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kocha wa Yanga, Marcio Maximo amesema atahakikisha wanasajili viungo mahiri katika kipindi kifupi kichacho cha usajili maarufu dirisha dogo.
Ikiwa chini ya kocha huyo za zamani wa Taifa Stars, Yanga tayari imeshapoteza mechi mbili msimu huu, sare moja na kushinda nne ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14.
Kabla ya kuondoka nchini kurejea kwao Brazil kwa ajili ya mapumziko.aximo ambaye Jumamosi kikosi chake kilishinda mechi ya raundi ya saba 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, amesema ana orodha ndefu ya viungo ambao kwa sasa wanahitajika Yanga.
“Tuko nafasi ya tatu katika msimamo kutokana na upungufu kidogo katika safu yetu ya kiungo. Usajili wetu wa dirisha dogo utajikita katika kuiongezea nguvu safu hiyo. Yanga ina washambuliaji na mabeki wengi lakini kuna upungufu katika kiungo,” amesema Maximo.
“Angalia idadi ya magoli tuliyofunga (magoli 9 katika mechi 7), ni wazi kwamba kuna tatizo kati ya viungo na washambuliaji wangu. Tunahitaji viungo wanaotengeneza nafasi nyingi za magoli kadri inavyowezekana.
MAXIMO
“Siwezi kukutajia wachezaji tunaowataka dirisha dogo, ni masuala yetu ya ndani hayo. Lakini ninachoweza kukuhakikisha kwa sasa kuna orodha ndefu ya viungo ambao nimependekeza uongozi uangalie uwezekano wa kuwapata walau wawili,” amesema zaidi Maximo.
Kiungo Jonas Mkude wa Simba ambaye leo anafanya maamuzi ya kusaini mkataba mpya wa miaka mitatu katika kikosi hicho cha Mzambia Patrick, anahusishwa mno na harakati za kukamilisha mipango ya Maximo ndani ya kikosi cha Yanga.
MSUVA, KIZZA KIKOSI CHA KWANZA
Aidha, raia huyo wa Brazil amekipongeza kikosi chake kwa kuikarisha Mgambo Shooting huku akiwamwagia sifa wachezaji watokea benchini, winga Simon Msuva aliyefunga magoli yote na mshambuliaji kutoka Uganda, Hamis Kizza.
“Msuva alicheza vizuri sana, Kizza pia ameimarika kwa kiasi kikubwa. Mara nyingi wamekuwa wakianzia benchi lakini ninaona kuna uwezekano mkubwa wa kuanza katika mechi ijayo (dhidi ya Azam FC Desemba 28),” ameongeza.
Simon aliyefunga magoli hayo dakika za 74 na 90, aliingia dakika ya 46 kuchukua nafasi ya kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ wakati Kizza alipishwa na beki wa pembeni Oscar Joshua dakika saba baada ya saa ya mchezo huku muuaji wa Stand United, Jerryson Tegete akichukua nafasi ya mshambuliaji kipenzi cha Maximo, Mbrazil Geilson Santos Santana ‘Jaja’ dakika ya 46.
“Jaja hakucheza vizuri kutokana na kuugua. Kizza aliona udhaifu wa Jaja, hakika amecheza vizuri lakini timu nzima imecheza vizuri. Niliona kuna haja ya kupunguza beki mmoja (Joshua) kwa sababu Mgambo walikuwa wazuri wa kucheza kwa kujilinda na walikuwa pungufu pia,” alisema.
Tangu kutua kwa Maximo mwishoni mwa Juni mwaka huu, Msuva na Kizza waliokuwa chaguo la kwanza la kocha Mholanzi Hans van der Pluijm aliyeondoka, wamekuwa wakisugulishwa benchi huku kocha huyo akiwapa nafasi Wabrazil wenzake Jaja na kiungo Andrey Coutinho anayemtumia kama winga.
KOCHA MGAMBO
Kocha wa Mgambo Shooting, Bakari Shime amesema kikosi chake kiliponzwa na maamuzi mabovu ya refa Ngole Mwangole kutoka Mbeya.
“Tangu kuanza kwa msimu huu, sijawahi kulaumu maamuzi ya marefa lakini mwamuzi wa mechi yetu dhidi ya Yanga mmh, niweke wazi hastahili kuchezesha ligi kama hii. Sijui TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) watachukua hatua gani maana walikuwapo uwanjani,” amesema Shime.
Ushindi wa Yanga ulichagizwa mno na maamuzi ya ovyo ya refa huyo, ambaye alionekana wazi kuifinyanga Mgambo JKT hasa alipoinyima penalti, mshambuliaji wake Malimi Busungu alipokwatuliwa na beki wa pembeni Juma Abdul ndani ya boksi la wanajangwani dakika ya 63.
Refa huyo aliionea zaidi Mgambo alipoacha kumlima kadi Abdul na kumwonesha kadi ya njano Busungu kwa madai kwamba alijiangusha. Refa pia hakuwatendea haki Mgambo katika goli la pili kwani kipa wao alifanyiwa rafu kabla Msuva hajapiga shuti kwenye lango lililokuwa tupu.
Yanga imepaa hadi nafasi ya tatu ya msimamo walipokuwa Azam FC ambao wameitoa Coastal Union nafasi ya pili. Azam na Yanga zote zina pointi 13 lakini wanalambalamba wanabebwa na mtiririko wa herufi.
 
Top