jaja 1
Kocha mkuu wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo ameamwagia sifa kiungo mkabaji Emerson De Oliveira Neves Rouqe huku akiutaka uongozi wa Yanga kusaka mechi mbili za kimataifa za kirafiki kabla ya kuivaa Simba Desemba 13 katika mechgi ya Nani Mtani Jembe 2 itakayopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Maximo mara tu baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam leo Jumatano alasiri, amedai Emerson ana uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa na atakuwa msaada mkubwa kwa Yanga kwa vile ni mzuri wa kupandisha mashambulizi na kuilinda timu kushambuliwa.
“Kabla sijarejea Brazil, nilisema Yanga ina washmabuliaji wengi lakini inahitaji viungo wenye uzoefu na wenye nguvu. Emerson ana sifa hizo ndiyo maana nimeamua kuja naye afanye kazi. Kinachofuata atazungumza na uongozi, kisha programu nyingine zitaendelea,” Maximo amesema.
“Jaja nimepata taarifa kwamba ana matatizo ya kifamilia na hataweza kuja tena Tanzania lakini bado sijapata rasmi taarifa kutoka kwake ama wakala wake.”

KUJIPIMA KIMATAIFA
Aidha, kocha huyo wa zamani wa Taifa Stars amesema ameuagiza uongozi wa Yanga kuhakikisha timu yake inapata mechi mbili za kimataifa za kirafiki kabla ya kuikabili Simba katika mechi ya ‘Nani Mtani Jembe 2′.
Emerson, mzaliwa wa Rio de Janeiro, anatarajiwa kuanza majaribio kesho Alhamisi, kabla ya kufanyiwa vipimo vya afya na kusajiliwa kuchukua nafasi ya Jaja, ambaye atakumbukwa kwa mabao yake mawili mazuri aliyofunga wakati Yanga ikiiadhibu Azam FC mabao 3-0 katika mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 14.
Katika mechi 11 ambazo Jaja alipangwa katika Kikosi cha Yanga, alifunga mabao sita, moja katika mechi saba zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na matatu katika mechi za kirafiki pamoja na mawili ya ‘video’ yaliyowapa wanajangwani Ngao ya Jamii.
 
Top