Match Report: Mtibwa Sugar 1- 1 Simba, Sare zazidi kuwaandama Wekundu wa Msimbazi
SARE ya 1-1 dhidi ya Simba iliyoipata Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Jamuhuri jioni hii imeifanya timu hiyo kuendelea kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania bara kwa kufikisha pointi 14 na kuiacha Simba ikipata sare ya sita msimu huu
Mtibwa Sugar inayonolewa na kocha Mecky Maxime ilipigana kufa na kupona hadi ikafanikiwa kusawazisha bao la mapema lililofungwa na nahodha wa Simba Josep Owino kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Mussa Hassan ‘Mgosi’ dakika ya 55
Simba ambao hawajaonya ladha ya ushindi tangu kuanza kwa msimu huu waliuanza mchezo huo kwa kasi na kulishambulia sana lango la Mtibwa kupitia kwa mshambuliaji wake Emmanuel Okwi na kufanikiwa kupata bao hilo lililodumu hadi mapumziko
Mtibwa wangeweza kwenda mapumziko wakiwa sawa na Simba baada ya kipa Manyika Peter kupangua mkwaju wa penati uliopigwa na beki David Luhende dakika ya 45.
Lakini pamoja na kukosa penati hiyo vijana wa kocha Maxime waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao Simba na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 55 kupitia kwa Mgosi aliyetumia vyema makosa ya kipa Manyika Peter ya kuudaka mpira na kisha kumponyoka ukampita tobo na kumuacha mfungaji akibaki peke yake na nyavu.
Katika mchezo huo pamoja na kutoka sare lakini Simba walionyesha kiwango cha juu kupitia kwa mshambuliaji wake Emmanuel Okwi na Ramadhai SIngano lakini walikosa bahati ya kutumbukiza wavuni mpira kila walipo jaribu kulisogelea lango la waopinzani wao.
Katika dakika ya 70 Simba iliwaingiza Uhuru Selemani, Amisi Tambwe na Abdalah Seseme kuchukua nafasi za Okwi,Elias Maguli na Awadhi Juma lakini wachezaji hao licha ya kupata nafasi nyingi za mabao walishindwa kubadilisha matokeo.
Kipigo hicho kinaifanya Simba kucheza mechi sita za Ligi msimu huu bila kupata ushindi katika hata mchezo mmoja.
Matokeo hayo yamezidi kumweka kocha Patrick Phiri na msaidizi wake katika hali ya hatari ya kupoteza kibarua chake baada ya mapema wiki hii uongozi wa Simba kumpa mechi mbili wakianza na hiyo ya Mtibwa na ya wiki ijayo dhidi ya Ruvu Shooting kubadilisha matokeo hayo ya sare.
 
Top