Klabu ya Simba SC ipo katika hatua za mwisho za kumrudisha nchini kwa mara ya tatu kocha, Milovan Curkovic. Msebria huyo ambaye aliinoa Simba kwa mara ya kwanza msimu wa 2007/08 akichukua nafasi ya Twalib Hilal, anachukuliwa kama suluhisho jipya la matatizo ya timu ndani ya uwanja. Mambo yamekuwa magumu kwa utawala mpya klabuni hapo. Msimu umeanza kwa tabu nyingi, mbinu za kocha Patrick Phiri zimekuwa zikipingwa hata kabla ya sare dhidi ya Mtibwa Sugar.
Wakati akirudi Simba kwa mara ya tatu , Phiri mshindi wa ligi kuu Tanzania Bara mara mbili ( 2005, na 2009/10, Mzambia huyo alipokelewa kwa ‘ mbwembwe’ nyingi na wanachama, mashabiki na baadhi ya viongozi wa timu hiyo. “ NImerudi Simba kurudisha mafanikio yaliyopotea” alisema Phiri mara baada ya kutua katika uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere, mwanzoni mwa mwezi Septemba.
Akitumia ‘ mwanya wa kusogezwa mbele kwa ligi kuu, Phiri alishahuri timu hiyo iweke kambi huko Visiwani, Zanzibar kujiandaa na msimu mpya. Wakati anaichukua timu hiyo kutoka kwa Mcroatia, Z. Logarusic, Simba tayari ilikuwa katika program ya msimu mpya kwa mwezi mzima. Awali timu hiyo ilianza kunolewa na kocha msaidizi, Suleimani Matola kabla ya Logarusic kuungana na timu baada ya kumaliza rikizo yake.
Logarusic aliingoza Simba kwa miezi sita, kabla ya kuhakikishiwa mkataba wa mwaka mmoja ambao ulikuja kuvunjwa baada ya mwezi mmoja kufuatia timu hiyo kutandikwa mabao 3-0 na Zesco United ya Zambia siku ya mchezo wa Tamasha la Simba Day-Siku maalumu ambayo klabu hiyo uitumia kutambulisha wachezaji wake wapya, mabadiliko ya jezi kuelekea msimu mpya na bidhaa mbalimbali za klabu.
Mwalimu, Loga alimrushia maneno makali kiungo, Shaaban Kisiga huku akimwambia ‘ amepelekwa tu klabuni hapo na si mchezaji bora ambaye ana hadhi ya kuichezea timu hiyo’. Loga kama, Mwalimu alijaribu kufanya usajili ambao alihitaji yeye tu. Hakupata sapoti ya moja kwa moja kutoka kwa wenyekiti wa kamati ya usajili Zacharia Hans Poppe ambaye alikuwa bize kusafiri huku na kule kusaka wachezaji aliosema ni ‘ bora’.
Uongozi mpya chini ya rais Evance Aveva na makamu wake Geofrey Nyange Kaburu wakatumia mchezo wa Simba Day kumuondoa Loga ambaye hadi sasa ameifungulia timu hiyo mashtaka katika Shirikisho la Soka la dunia, FIFA akidai zaidi ya Milioni 90, ambazo Simba watawajibika kumlipa kwa kuvunja mkataba baina yao. Loga alitajwa mtu hasiyeweza kuishi vizuri na wachezaji wake, mtu wa starehe kuliko kazi. Alifukuzwa kazi huku akiwa ametoka kukataa kazi ya maana nchini Kenya sehemu ambayo alishinda ubingwa wa KPL.
Kuondolewa kwa Logarusic kulichukuliwa na kuonekana kama mwanzo wa kuinua hali ya ushindi katika timu hiyo ambayo haijafanikiwa kushinda mchezo wowote wa kimashindano tangu mwezi Machi ilipoifunga Ruvu Shooting, timu ambayo watacheza nayo katika raundi ya saba mwishoni mwa wiki ijayo. Phili aliyezaliwa mwaka 1956 ni kocha aliyekomaa katika kazi yake, labda amerudi Simba katika wakati mbaya.
Mshambulizi huyo wa zamani wa Zambia ambaye alicheza michuano ya AFCON, 1978 na ile ya 1982 ni kocha mwenye sifa ya kushinda mataji mengi. Phiri ameshinda mataji 12 tofauti, mataji kumi akishinda akiwa katika ngazi ya ufundishaji wa klabu na mengine mawili alishinda wakati akiionoa timu ya Taifa ya Zambia. Mataji ya Cosafa Cup na Cecafa Cup, mwaka 2006 ndiyo pekee ambayo kocha huyo ameyashinda kama mwalimu.
Mara mbili ametwaa mataji ya ligi kuu ya Zambia, 1999 na 2001, mara mbili ameshinda mataji ya ligi kuu Tanzanis Bara, 2004 na 2009/10, Zambia Cup, 2000, BP Top8, 1997 na 1998 na 2000, Phiri pia ametwaa mataji ya Tusker Cup akiwa na Simba, 2005 na ametwaa taji la Ngao ya Jamii, 2000 nchini Zambia hivyo chaguo la uongozi wa Simba lilikuwa sahihi. Simba ilihitaji mtu anayeifahamu zaidi timu hiyo kuliko kocha bora zaidi, lakini mambo yamekuwa sivyo kwa sababu kocha huyo amekuwa akiingiliwa katika kazi yake mara tu baada ya kuanza kwa msimu.
Wakati wa harakati za uchaguzi mkuu wa klabu hiyo katikati ya mwaka huu, Makamu wa sasa wa rais wa timu hiyo ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo na kushinda, aliniambia kuwa Simba inahitaji kuwatengeneza wachezaji wake yenyewe kwa madai kuwa ‘ soka la Tanzania linachezwa hadi nje ya uwanja’. Akitolea mifano ya wachezaji vijana kama Ramadhani Singano, Jonas Mkude, Abdallah Seseme, Hassani Isihaka, Miraj Adam, Kaburu alimzungumzia sana kocha Milovan kuwa ni mtu ambaye anaweza kuifanya Simba kufanikiwa.