Mgambo Shooting ya Tanga ilifanikiwa kupata ushindi wa tatu msimu huu katika ligi kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa, Mbeya City kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kukamilisha raundi ya sita ya michezo ya ligi kuu. Mgambo imeruka kutoka nafasi ya 12 hadi katika nafasi ya sita ya msimamo nyuma ya vinara Mtibwa Sugar kwa tofauti ya pointi tano. Kikosi cha kocha Bakari Shime kipo nyuma ya Coastal Union iliyo katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi mbili, huku wakizidiwa na timu za Azam FC, Yanga SC kwa pointi moja.
Mgambo wamelingana pointi na Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tano wakifungana kwa pointi tisa kila mmoja…. Vinara Mtibwa chini ya kocha Mecky Mexime wamekuwa katika kiwango kizuri hadi sasa. Ikiwa haijapoteza mchezo wowote, kwa mara ya kwanza msimu huu timu hiyo ilitanguliwa kufungwa katika mchezo lakini waliweza kusawazisha katika mchezo dhidi ya mabingwa mara 19 wa zamani, Simba SC katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mtibwa imefunga mabao tisa na kuruhusu mabao mawili tu katika nyavu zao. Ushindi mkubwa zaidi kwa timu hiyo ni ule wa raundi ya pili walipoichapa, Ndanda FC ya Mtwara kwa mabao 3-1 katika uwanja wa Manungu Complex, ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga na Mbeya City katika uwanja wa Sokoine, Mbeya umeleta picha mpya msimu huu kuwa mabingwa hao wa miaka ya 1999 na 2000 wamepania kufanya kweli msimu huu. Timu iliyomaliza katika nafasi ya nane msimu uliopita imerudi ikiwa na nguvu, hali, mbinu, na ufundi zaidi.
Coastal Union wamekuja ‘ kivingine’ kabisa msimu huu. Coastal imepoteza mara moja katika michezo sita iliyokwishacheza. Jambo kubwa walilofanya msimu huu ni kutengeneza idara yao ya ufundi kwa umakini mkubwa. Yusuph Chippo na wasaidizi wake, Bernard Mwalala, na Razaq Siwa wapo makini sana, wanafanya kazi katika sehemu ambayo hawapati presha kutoka kwa uongozi wao. Kitu muhimu ni kwamba walimu hao wote ni raia wa Kenya na wapo Tanzania kusaka mafanikio katika kazi yao.
Kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa City kati ka uwanja wa Sokoine hakikuwarudisha nyuma, ikiwa imetoa sare mara mbili tena ikicheza katika viwanja vya ugenini ( dhidi ya Simba na Kagera Sugar), Coastal imeonekana kuimarika na kufanya vizuri katika uwanja wa nyumbani. Walishinda dhidi ya Mgambo, na Ndanda FC kabla ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuishinda Ruvu Shooting. Coastal ndiyo timu pekee iliyofanikiwa kushinda michezo yote katika uwanja wa nyumbani msimu huu.

Msimu uliopita timu hiyo ilikuwa na wachezaji wengi wenye majina makubwa lakini walimaliza katika nafasi ya tisa, jambo ambalo lilifanya wajipange kwa msimu huu. Ramadhani Salim mmoja wa washambuliaji watatu wa kigeni katika timu hiyo kutoka nchini Kenya amefanikiwa kufunga mabao matatu kati ya magoli waliyofunga timu nzima msimu huu. Kitu pekee ambacho, Chippo na wasaidi wake wanatakiwa kukitilia mkazo hivi sasa ni idara ya ulinzi ambayo imeruhusu mabao matano katika michezo sita iliyochezwa.
Didier Kavumbagu alifunga mabao manne katika michezo miwili ya mwanzo, lakini hajafunga tena na timu imekosa makali katika ufungaji. Azam wana wastani wa mabao matatu baada ya kucheza michezo sita. Wamefunga magoli sita tu licha ya kuwa na idadi kubwa ya washambuliaji wa kigeni. Kipre Tchetche, Leonel Saint, Ismael Diarra na Kavumbagu wote hao ni wachezaji wa kigeni kutoka nchi za Ivory Coastal, Haiti, Mali na Burundi, pia kocha Mcameroon, Joseph Omog ana wigo mpana wa kuchagua washambuliaji.
Hamis Mcha, Gaudensi Mwaikimba ni wazawa ambao wanaweza kuisaidia timu hiyo kupata mabao wakati wachezaji wengine kama, nahodha, John Bocco na Kelvin Friday wakiendelea vizuri kupona majeraha yao. Vipigo kutoka kwa JKT Ruvu na Ndanda FC vinaweza kuonekana si tatizo lakini ukweli hiyo ni dalili ya kuanza kuchoka kimbinu na kiufundi.
Msimu uliopita timu hiyo ilishinda michezo sita na kutoa sare mara saba katika michezo 13 ya mzunguko wa kwanza, na walishinda michezo 11 na kutoa sare mara mbili katika michezo 13 ya mzunguko wa pili. Azam walimaliza msimu bila kupoteza mchezo wowote. Walikuwa bora na wamoja, nini kinawakuma hivi sasa?. Bado wana nafasi ya kubadilisha mambo na kufanya vizuri kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini mambo hayatakwenda kiuwepesi kama walivyotwaa taji bila kupoteza mchezo.
 
Top