Mshambulizi wa klabu ya Simba SC, Mrundi, Amis Tambwe alifunga mabao 19 na kutwaa kiatu cha dhahabu kama mfungaji wa ligi kuu Tanzania Bara, msimu wa 2013/14. Katika msimu ambao Simba ilipata matokeo mabaya zaidi na kumaliza katika nafasi ya nne, Tambwe ambaye mara nyingi alipangwa kama mshambulizi wa kwanza alikuwa na mafanikio binafsi katika mdsimu wake wa kwanza tu katika ligi ya juu nchini.
Ni mshambulizi wa kwanza wa kigeni katika ‘ karne mpya’ kufunga mabao mengi katika msimu wake wa kwanza. Mabao yake mawili katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar mwanzoni mwa msimu yalimtambulizi kama ‘ mfungaji wa hatari’ akiwa ndani ya eneo la hatari. Alifunga ‘ hat-trick’ mara mbili katika michezo 23 aliyocheza. Betram Mwombeki alikuwa msaidizi wa Tambwe, baadaye Mrundi huyo akawa akipangwa na wachezaji tofauti katika safu ya mashambulizi.
Tambwe hakufunga sana katika michezo ya mzunguko wa pili na jambo hilo limeendelea katika msomu huu. Msimu ulionekana kama ungekuwa mzuri kwa mshambulizi huyo baada ya kufunga bao katika mchezo wa kwanza tu msimu huu. Akicheza sambamba na Emmanuel Okwi katika safu ya mashambulizi, Tambwe alifunga katika mchezo wa sare ya kufungana mabao 2-2 na Coastal Union siku ya ufunguzi.
Alipangwa tena na Okwi katika mchezo uliofuata dhidi ya Polisi Morogoro. Bao la kwanza kwa msimu safari hii lilikwenda kwa Okwi, lakini timu iliambulia sare nyingine. Baada ya mchezo huo dhidi ya Polisi Moro tetesi zilianza kuvuja kuwa washambuaji hao wa kigeni ‘ haivi’. Tambwe alijiunga Simba msimu uliopita akitokea Vitao’o ya Burundi na kusaini mkataba wa miaka miwili amekosa furaha . Huku mshahara mkubwa anaopata Okwi ukitajwa kama sehemu ya kiwango chake cha chini msimu huu.
Okwi ambaye amesajiliwa kwa mkataba wa muda mfupi, anaingiza kibindoni kiashi cha Tsh. 4.5 milioni, wakati Tambwe anaingiza mshahara wa usiozidi Tsh. 2 milioni. Tambwe alicheza kwa kiwango cha chini katika mchezo dhidi ya Stand United ambao pia ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1. Bao la mkwaju wa faulo kutoka kwa Shaaban Kisiga lilifutwa na Stand katika mchezo ambao, Okwi na Tambwe hawakufanya vizuri.
Katika gali isiyotarajiwa, Tambwe aliwekwa benchi katika mchezo dhidi ya Yanga SC na nafasi yake ilichukuliwa na Elius Maguli. Yanga na Simba hazikufungana katika mchezo huo lakini kitendo cha kuwekwa benchi kwa mchezaji huyo kilimuumiza, huku mashabiki wakijiuliza kwa nini?. Patrick Phiri alimrudisha katika kikosi cha kwanza mshambuaji huyo mwenye sifa ya kufunga maao ya kichwa. Tambwe na Okwi wakapangwa katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ulikuwa ni mchezo wa tano kwa Simba msimu huu, na wawili hao walianza kwa wakati mmoja kwa mara nyingine na ilionekana kama mambo yatakuwa mazuri baada ya Okwi kufunga bao la kuongoza kwa Simba katika dakika ya tano tu ya mchezo. Lakini hakuna tena walichoweza kufanya, Prisons walisawazisha katika dakika za mwisho na kutengeneza sare ya kufungana bao 1-1. Hakuna aliyesema, Okwi alililia sana baada ya mchezo huo dhidi ya Prisons hiyo ilikuwa dalili mbaya, dalili ya kutokufanikiwa .
Katika michezo sita iliyocheza msimu huu, Simba imefanikiwa kufunga mabao sita tu, huku mfungaji bora katika timu akiwa amefunga bao moja na mchezaji mwenye thamani zaidi akiwa amefunga mabao mawili. Kisiga mchezaji wa nafasi ya kiungo amefunga mabao mawili, yote kwa mipira iliyokufa, huku bao lingine likiwa limefungwa na mlinzi na nahodha wa timu, Joseph Owino katika mchezo wa sare ya kufungana bao 1-1 kati ya Mtibwa Sugar na Simba mwishoni mwa wiki iliyopita.
Habari za chini chini zinadai kuwa Tambwe anaweza kuondoka katika timu hiyo, hilo linachochewa na kiwango chake katika siku za karibuni. Yule mfungaji ‘ bingwa wa mabao ya kuvuzia’ amekuwa butu msimu huu wakati ameingezewa wasaidizi wa kutosha. Tambwe ni mshambuaji ambaye anatakiwa kupewa kipau,bele katika kikosi cha Simba, inadaiwa kuwa ‘ ametengwa’ huku uongozi ukiwekeza kila kitu kwa Okwi. Atakapoanza kucheza Paul Kiongera bila shaka, Tambwe atakuwa sokoni hata kwa mkopo.
            
 
Top