Kuingia katika vitabu vya historia kama kocha pekee kuiongoza timu ‘ mwanzo-mwisho’ kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara bila kupoteza mchezo wowote akiwa na kikosi cha Simba SC, 2009/10 lilikuwa jambo la kujivunia sana kwa kocha, Mzambia, Patrick Phiri. Mchezo kati ya Simba na Ruvu Shooting siku ya Jumapili ulimalizika furaha kubwa, mashabiki, wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wote walikuwa ‘ katika sikukuu ya klabu’
Simba ilicheza michezo 12 mfululizo ya ligi kuu pasipo kushinda. Mara ya mwisho walipata ushindi miezi Saba iliyopita walipoishinda, Shooting kwa mabao 3-2. Baada ya ushindi wa kwanza katika michezo saba msimu huu, Simba imekata kiu ambayo walikuwa nayo kwa muda mrefu. Kila mtu klabuni hapo alihitaji kujisikia kuna kitu fulani kikubwa cha kupanga kukipata. Unaweza kuishi bila lengo kubwa kwa mwaka mmoja, lakini kimsingi Simba ilikosa raha kwa kuwa na hali ya kutokuwa na malengo makubwa.
Emmanuel Okwi alifunga bao lake la tatu msimu huu zikiwa zimesalia dakika 11 mchezo kumalizika. Okwi, nahodha, Joseph Owino, Uhuru Suleimani ni baadhi ya wachezaji walioshinda ubingwa bila kupoteza miaka minne iliyopita. Licha ya kuanza ligi kwa mwendo wa kusuasua, Simba inaonekana itarudi na kuwa timu tishio msimu huu kutokana na kuwa nyuma ya pointi tano dhidi ya vinara, Mtibwa Sugar. Huku zikiwa zimesalia mechi sita kukamilika kwa mzunguko wa kwanza, Simba inaweza kuwa juu zaidi ya ilipo sasa.
Timu ilicheza mpira mzuri sana dhidi ya Shooting. Nafikiri kilikuwa kiwango cha hali ya juu kuliko vyote vilivyoonekana msimu huu. Hakika walicheza vizuri, na walistahili kupata ushindi wa kwanza. Hiki ni kipindi kizuri sana kwa wachezaji ambao hawakuficha furaha waliyokuwa nayo mara baada ya mwamuzi kumaliza mchezo. Ilikuwa mechi yenye presha kubwa, Phiri angefukuzwa kazi endapo timu ingepoteza au kupata sare ya saba mfululizo.
Phiri amekuwa akisema ana kikosi cha hali ya juu lakini hata yeye alikuwa hajui kwa nini hawapati ushindi licha ya kutangulia kufunga katika michezo mitano kati ya sita waliyotoa sare.
Bao la Okwi lilikuja baada ya ‘ muunganiko mzuri wa timu’. Elius Maguli alipiga kiki ambayo, Okwi aliifuatilia na kuukuta mpira unarudi na kufunga. Hali hiyo ya kusaka bao ilioneshwa na wachezaji ilikuwa kama kumtetea kocha wao asitimuliwe, na walifanikiwa.
Bao la Okwi lilikuja baada ya ‘ muunganiko mzuri wa timu’. Elius Maguli alipiga kiki ambayo, Okwi aliifuatilia na kuukuta mpira unarudi na kufunga. Hali hiyo ya kusaka bao ilioneshwa na wachezaji ilikuwa kama kumtetea kocha wao asitimuliwe, na walifanikiwa.
Tangu aliporejea klabuni hapo kwa mara ya tatu, Phiri alisema kuwa anaheshimika sana katika timu ya Simba na mara zote anajihisi klabuni hapo ni kma nyumbani kwake. Phiri ameruka kikwazo cha kutimuliwa na kuwa miongoni mwa walimu wawili ambao hawajapoteza mchezo msimu huu sambamba na Mecky Mexime wa Mtibwa. Aliacha kusikiliza hisia zake na kutazama mambo katika mtazamo wa kisoka na kutafakari kama matamanio yake na matamanio ya klabu yanaoana. Sasa ana uhakika wa asilimia mia kuwa atabaki klabuni hapo na kuendelea kufanya kazi yake. Baada ya ushindi wa kwanza baada ya mechi 13, sasa, Simba wanatakiwa kuwa na malengo makubwa.