IMG_8708.JPG
BAADA ya kukaa miezi nane bila kupata ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Simba imezinduka na kuichapa timu ‘iliyoiroga’ Ruvu Shooting bao 1-0 katika mechi ya raundi ya saba iliyochezwa, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jioni hii.
Simba iliyoambulia sare katika michezo yake yote sita iliyopita, mara ya mwisho kupata ushindi ilikuwa pale ilipoinyuka mabao 3-2 timu hiyo ya kocha Mkenya Tom Olaba kwenye Uwanja wa Taifa miezi nane iliyopita. Baada ya hapo Simba ilicheza mechi 12 bila ushindi ikipigwa na kutoka sare.
Bao pekee katika mechi ya leo limefungwa na mshambuliaji wa kimataifa kutoka Uganda, Emmanuel Okwi ambaye amecheza mechi ya nne Simba akiwa mgonjwa.
Okwi, amemalizia mpira wa shuti kali la mtokea benchini Elias Maguli lililotemwa na kipa Abdallah Rashid wa Ruvu Shooting na kuwanyamazisha mashabiki wa Yanga waliokuwa wakimzomea uwanjani kipindi chote kabla ya kufunga.
Mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi la Simba chini ya Mzambia Patrick Phiri kwa kumtoa kiungo Said Khamis na kumuingiza Maguli dakika saba baada ya saa ya mchezo, yameleta uhai katika kikosi cha Wanamsimbazi kwani mshambuliaji huyo alionekana kuujua udhaifu wa timu yake ya zamani, Ruvu Shooting.
Kocha Olaba amefanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwatoa mshambuliaji Juma Mtindi na winga Raphael Keyala na kuwaingiza Juma Seif na Seif Abdallah lakini mabadiliko hayom hayakuzaa matunda mema kwa kikosi chake.
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kililazimika kufanya kazi ya zaida kuwadhibiti mashabiki wa Simba waliokuwa wamekizunguka kikundi cha mashabiki wengine wa klabu hiyo wanaodaiwa kuwa ni waasi ‘Simba Ukawa’ nje ya Uwanja wa Taifa.
okwii
Simba iliyokuwa ikicheza mechi ya tano kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu, ilienda mapumziko ikiwa haijafanya shambulizi lolote la maana langoni kwa wapinzani zaidi ya kusababisha kona nane ambazo hazikuzaa matunda, hata hivyo.
Okwi alipata nafasi nne za wazi kipindi cha kwanza, lakini alishindwa kuipatia mabao timu yake dakika za 8, 18, 32 na 40.
Katika kipindi hicho, Simba ilipata kona nane dakika za 7, 15, 34, 35, 37, 41, 42 na 45 lakini wachezaji wake walionesha wazi kutokuwa wazuri katika kumalizia mipira ya aina hiyo.
Kipindi cha kwanza Simba pia ilipiga mashuti nane ambayo hayakuzaa mabao hata hivyo huku wageni wao, Ruvu Shooting wakipiga mashuti manne ambayo hayakuwa na madhara pia.
Shambulizi kali zaidi la Ruvu Shooting lilifanywa dakika tatu kabla ya mapumziko krosi ya Abdulrahman Musa ilipotua kwenye guu la kulia la mshambuliaji Mathayo Wilson lakini umahiri wa kipa Ivo Mapunda ukaiokoa Simba kufungwa goli.
Kichwa cha mshambuliaji Juma Mdindi dakika ya 28 kilimpita kipa Ivo lakini Nahodha wa Simba, Mganda Joseph Owino aliuwahi mpira na kuokoa hatari hiyo langoni kwao.
Vikosi vilikuwa:
Simba: Ivo Mapunda, William Lucian, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Awadh Juma/ Abdallah Seseme (dk 90), Amissi Tambwe, Said Khamis/ Elias Maguli (dk 67) na Emmanuel Okwi.
Ruvu Shooting: Abdallah Rashid, Said Madega, Yusuph Nguya, Frank Msese, Salvatory Ntebe, Zubeiry Dabi, Raphael Keyala/ Seif Abdallah (dk 63), Juma Made, Mathayo Wilson, Juma Mdindi/ Juma Seif (dk 48) na Abdulrahman Musa.
 
Top