1. STAND UNITED YASHINDA NYUMBANI
Raundi ya saba ilishuhudiwa timu mpya VPL Stand United kutoka Shinyanga ilipata ushindi wake wa kwanza nyumbani ilipoinyuka Mbeya City bao 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Mechi hiyo ilifuta rekodi mbaya ya timu hiyo ya usukumani kucheza mechi sita za VPL bila kupata ushindi kwenye uwanja wake wa nyumbani.


Stand ilifungwa 4-1 dhidi ya Ndanda FC katika mechi yake ya kwanza kwenye uwanja huo msimu huu, ikafungwa 3-0 na Yanga kabla ya kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Mbeya City iliyoko mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo.
Stand ilicheza mechi tatu ugenini ikishinda moja (1-0) dhidi ya Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ikaambulia sare dhidi ya Simba (1-1 Uwanja wa Taifa), Kagera Sugar ( 0-0 Uwanja wa Kaitaba) huku ikipata sare ya bao moja pia nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.
Goli lao la ushindi katika raundi ya saba iliyochezwa Novemba 8, mwaka huu Mbeya City kwenye Uwanja wa Kambarage, lilifungwa na mshambuliaji Mnigeria Abasirim Chidiebere dakika mbili kabla ya mechi kumalizika.
2. SIMBA YAONA MWEZI
Simba iliona mwezi baada ya kupata ushindi wake wa kwanza VPL baada ya kukaa siku 252 bila kupata ushindi. Simba waliifunga timu ‘iliyowaroga’ ya Ruvu Shooting bao 1-0 kwenye mechi ya raundi ya saba iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Mara ya mwisho Simba kupata ushindi ilikuwa dhidi ya timu hiyo hiyo ilipoifunga 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa miezi nane iliyopita tangu Machi 2, mwaka huu. Baada ya hapo walipigwa na kuambulia sare.
Goli la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji wao kutoka Uganda, Emmanuel Okwi likiwa ni bao lake la tatu msimu huu baada ya kufunga pia dhidi ya Polisi Morogoro na Prisons.
Simba chini ya kocha wake Mzambia Patrick Phiri ilikuwa imecheza mechi sita bila kupata ushindi wowote msimu huu baada ya kuambulia sare katika mechi zote sita za awali.
Ushindi huo pia ulikuwa wa kwanza baada ya mechi kucheza mechi 12 bila ushindi VPL.
3. MTIBWA, KAGERA WACHEZA SIKU MBILI
Mechi ya raundi ya saba kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya ndugu zao Kagera Sugar nayo iliingia kwenye rekodi ya kukumbukwa kwenye VPL msimu huu baada ya kuchezwa kwa siku mbili katika Uwanja wa Manungu, Turiani KM 100 kutoka mjini Morogoro.
Ni mechi ya kwanza ya Ligi Kuu kuchezwa kwa siku mbili nchini kwani kabla ya tukio hilo, mechi nyingi zilikuwa zikiahirishwa kabla ya kuanza na kuchezwa siku nyingine.
Mechi hiyo ilichezwa Jumamosi ya Novemba 8 kwa dakika 45, lakini marefa wakaamua kuisimamisha kutokana na mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo.
Hadi mechi inavunjwa, wenyeji Mtibwa walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wao hatari msimu huu Ame Ally Amour dakika mbili kabla ya mechi hiyo kwenda mapumziko na baadaye kusimamishwa.
Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) toleo la 2014, mechi hiyo ilichezwa kesho yake asubuhi kumalizia dakika 45 zilizokuwa zimebaki na Kagera Sugar walifanikiwa kusawazisha bao ililofungwa kupitia kwa mshambuliaji wao, Rashid Mandawa dakika nne kabla ya saa ya mchezo (dakika ya 56) na kuifanya mechi hiyo ya aina yake kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Hilo klilikuwa goli la tatu kwa Mandawa msimu huu.
4. MBEYA CITY YAPOTEZA MECHI YA NNE MFULULIZO
Raundi ya saba imeshuhudiwa pia Mbeya City iliyofanya vizuri msimu uliopita ikimaliza nafasi ya tatu ikipoteza mechi yake ya nne mfululizo ilipofungwa 1-0 dhidi ya Stand United usukumani mjini Shinyanga.
Msimu uliopita, Mbeya City ilipoteza mechi tatu tu ikifungwa na mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, Yanga, mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union na mabingwa wapya wa VPL, Azam FC, hivyo kwa kuifunga Mbeya City Novemba 8, Stand United wamevunja rekodi ya mechi za Mbeya City kupoteza msimu uliopita.
‘Majanga ya Snura’ yalianza kuikumba Mbeya City kwenye mechi za raundi ya nne ilipokubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani Sokoine dhidi ya Azam FC, ikabamizwa mabao 2-0 kwenye uwanja huo huo dhidi ya vinara Mtibwa Sugar, ikipigwa 2-1 na Mgambo mjini Tanga kabla ya kukutana na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Stand United.
5. MAGOLI 91 MECHI 49
Raundi ya saba pia ilishuhudiwa mabao 91 yakifungwa katika mechi 49 za raundi zote saba msimu huu ikiwa ni wastani wa 1.86. Mabao 50 yalifungwa na timu zilizokuwa nyumbani huku timu ngeni zikifungha mabao 41 ikitoa taswira kwamba timu bado zuina desturi ya kutumia vyema viwanja vyake vya nyumbani. Yanga ndiyo wametia fora kwa kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwani katika mechi zote nne walizocheza nyumbani wameshinda tatu na kupata sare moja dhidi ya Simba.
Msimu uliopita hadi raundi ya saba yalikuwa yamefungwa mabao 101 ikiwa ni wastani wa mabao mawili kila mechi. Mfungaji bora wa msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe hadi raundi hii alikuwa amefunga mabao nane ikiwa ni sawa na mabao ambayo timu za Azam, Simba na Ndanda FC zimefunga katika raundi zote saba zilizopita.
6. MWAMBUSI AACHIA NGAZI
Wiki moja baada ya mechi za raundi ya saba, Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alitangaza kuachia ngazi kuinoa timu hiyo pendwa mkoani Mbeya kutokana na kile alichokiita kusakamwa huku viongozi wakielewa fika kinachopitafuna timu hiyo msimu huu.
Uongozi wa klabu hiyo umesema utatoa ufafanuzi kuhusu jambo hilo wiki ijayo na unaendelea kumtambua Mwambusi kama kocha wake mkuu.
7. SURE BOY ALAMBA TUZO
Mechi ya raundi ya saba kati ya Azam FC na Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam uliopo Mbande jijini Dar es Salaam, ilishuhudiwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy akiakabidhiwa tuzo yake ya mchezaji bowa wa mwezi Oktoba akilamba Sh. milioni moja na kikombe cha heshima.
Kiungo Antony Matogolo wa Mbeya City ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mwezi Septemba akiwa ndiye mchezaji wa kwanza kupokea tuzo hiyo tangu ianzishwe msimu huu.

Baadhi ya wadau wamekuwa wakilalamikia utaratibu unaotumika kwa maana mchezaji bora inafikia kipindi anapewa baada ya kucheza mechi mbili tu mfano Septemba (Matogolo) na Novemba (bado hajatajwa).

 
Top