MSHAMBULIAJI Amissi Tambwe wa Simba aliyefulia kwa mabao msimu huu, amesema anaendelea kuheshimu mkataba wake na klabu hiyo na hana mpango wa kutimkia kwingineko kwa sasa.
Tambwe, ambaye amefunga bao moja tu katika mechi tano alizopangwa katika Kikosi cha Simba msimu huu, amekuwa akidaiwa kutaka kuihama timu hiyo ya Msimbazi kutokana na kinachoelezwa kutoheshimiwa na baadhi ya viongozi.
Tambwe, mfungaji bora wa VPL msimu uliopita na mfungaji bora wa Kombe la Kagame mwaka jana, hakupangwa katika mechi iliyopita ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga kwa maelezo yaliyotolewa na Kocha Mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri kuwa hana uwezo wa kukabiliana na mabeki wenye nguvu kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani wa Yanga.
DSC_0901
Akizungumza na mtandao huu kwa simu leo mchana akiwa katika kambi ya timi hiyo jijini, Tambwe amesema: “Bado niko Simba na nitaendelea kuwa Simba ingawa mambo si mazuri sana kwangu kwa sasa kimpira.”
Tambwe amekiri kuandamwa na baadhi ya watu ndani ya kikosi hicho kilichopoteza ghafla matumaini ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, kikiambulia sare katika michezo yote sita kiliyocheza.
Baada ya timu yao kutoka sare ya bao moja dhidi ya Tanzania Prisons Oktoba 25, uongozi wa juu wa Simba uliwasimamisha viungo Amri Kiemba na Shaban Kisiga pamoja na winga Haroun Chanongo huku Tambwe akiwa nmi miongoni mwa wachezaji waliopewa onyo kwa madai kuwa hawajitumi.
Tambwe aliyefunga goli lake pekee msimu huu dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Oktoba 21, alijiunga na Simba Agosti mwaka jana alitokea kuipa ubingwa wa Kombe la Kagame Timu ya Vital’O ya kwao Burundi.
Simba iko kambini jijini Dar es Salaam tangu mwanzoni mwa wiki kujiandaa kwa mechi yake ya raundi ya saba dhidi ya Ruvu Shooting itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili.
 
Top