UONGOZI wa Yanga umesema bado haujapokea ofa yoyote kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba kumsajili winga Simon Msuva aliye katika matawi ya juu kwa sasa licha ya kuonekana wazi kubaniwa na kocha mkuu wa Wanajangwani, Mbrazil Marcio Maximo.
Aidha, uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani umejibu vijembe vya Mwenyejiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope kwa kusema kuwa kiongozi huyo wa Simba ni mwanachama, tena wa kadi wa Yanga.
Wiki iliyopita Simba baada ya kufanikisha kumbakisha kiungo wake mkabaji Jonas Mkude kwa kumsainisha mkataba mpya wa miaka miwili, ulisema kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati yake ya Usajili, Hanspope kuwa utawasilisha ofa kwa Yanga kumsajili Msuva kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.
Usajili wa dirisha dogo ulifunguliwa rasmi juzi Jumamosi na utafungwa rasmi Desemba 15, mwaka huu.
Hata hivyo, Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Beno Njovu wamesema jijini Dar es Salaam leo kuwa bado hawajapata barua yoyote kutoka Simba kuhusu winga huyo aliyefunga mabao mawili katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) waliyoshinda 2-0 dhidi ya Mgambo Shooting.
“Hakuna barua yoyote kutoka Simba inayotuomba wamsajili Msuva. Hanspope aliongea kuhusu suala hilo ili kuwafurahuisha walionuna. Na sisi tunajibu vijembe vyake kwa kuwataarifu Simba kwamba Hanspope ni mwanachama wa Yanga, tena wa kadi. Nimekosa tu kijana wa kumtuma aniletee nakala ya kadi yake ambayo klabu inayo,” amesema Njovu.
“Hawana nia thabiti ya kumsajili Msuva ndiyo maana Hanspope alisema ofa aliyonayo kumsajili mchezaji wetu ni Sh. 500,000, huo ni utani,” ameongeza.
Akitangaza nia hiyo mbele ya waandishi wa habari, Hanspope alisema: “Mkude ameamua kubaki Simba kwa sababu hawezi kwenda Yanga kucheza ufukweni kama alivyotamba Manji (Yusuph) kwamba ana uwezo wa kusajili wachezaji wiote wa Simba na kuwapeleka ufukweni kucheza soka. Mkude anataka kucheza uwanjani na si ufukweni.”
 
Top