KIKOSI cha ‘maafande’ wa Ruvu Shooting kimepata pigo baada ya wachezaji wake saba kukacha soka na kutimkia kwenye mafunzo ya kijeshi, imefahamika.
Msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire amesema jijini leo kuwa wachezaji hao, ambao wengi wao ni washambuliaji, wamelazimika kuachana na soka kwa muda ili kupata mafunzo hayo ikiwa ni taratibu kuelekea kupata ajira za kijeshi. Ruvu Shooting inamilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kupitia Kitengo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Ni jambo la kawaida, wachezaji wanakwenda kwenye shughuli nyingine za nje ya soka. Katika wachezaji 30 wameondoka hao saba, kikubwa hatufanyi usajili wa kibabaishaji, kikosi chetu bado kiko imara,” amesema Bwire.
“Kwa sasa siwezi kuwataja kwa majina kwa sababu ni mapema mno. Wachezaji wetu lakini wengi ni washambuliaji na kocha ameagiza tusajili washambuliaji wawili dirisgha dogo ili wasaidiane na washambuliaji wachache waliobaki,” amesema Bwire.
Msimu uliopita, baadhi ya wachezaji wa timu hiyo walitimkia Uarabuni kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa ughaibuni, jambo ambalo hawakufanikiwa, hata hivyo.
 
Top