Kutokana na mchango mdogo ambao ameuonesha katika michezo ya msimu huu, klabu ya Simba SC imelazimika kumuuza kwa uhamisho wa mkopo kiung-mshambulizi, Amri Kiemba Ramadhani, 31 kwa timu ya Azam FC. Simba wamesema kuwa ni uamuzi wa kawaida tu ambao wameufanya na wala si maamuzi ya kukurupuka ambayo yamemuondoa mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kiemba alijiunga na Simba katikati ya mwaka 2009 akitokea Moro United tayari ameanza mazoezi na klabu yake mpya ambayo imemsaini kwa lengo la kuongeza changamoto, uwezo na uzoefu kwa mabingwa hao wa Tanzania Bara ambao watacheza kwa mara ya kwanza katika ligi ya mabingwa Afrika hapo mwakani.
Azam imedhamiria kufanya vizuri katika michuano hiyo, kufika hatua ya makundi ni ‘ target’ ya kwanza, hivyo usajili wa wachezaji wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa kama Paschal Serge Wawa, Kiemba ni sehemu ya kuhakikisha ‘ ujenzi wa timu bora zaidi’ kuelekea michuano hiyo ukifanyika kwa uhakika.
Achana na habari kuwa mchezaji huyo wa nafasi ya kiungo hana nidhamu, katika msazingira ya klabu yake ya zamani ( Simba) tayari walikwisha mchoka, lakini kiuchezaji, kinidhamu, na kiuwajibikaji, Kiemba ni mchezaji ambaye alihitaji changamoto mpya,. Azam ni sehemu ambayo anaweza kufanya kazi akiwa huru kuliko Simba.
Akiwa ameiwakilisha, Stars mara 14 katika michezo ya FIFA katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mchezaji huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga SC na Miembeni FC , Kiemba ni mkali wa mbinu, ana macho katika utoaji wa pasi, kila mtu anatambua kuwa Kiemba ni mmoja kati ya viungo bora nchini katika kipindi cha miaka miwili na nusu sasa.
Kiemba ni mjanja na mchezaji mwenye akili sana awapo uwanjani, Azam haijafikiria sana uwepo wa viungo-bora kama Himid Mao, Salum Abubakary, Kipre Bolou, Frank Domayo zaidi wanahitaji kuwa na kikosi kikubwa ambacho kinaweza kutimiza sehemu ya malengo yao katika michuano ya kimataifa na ile ya ndani ya nchi.
Joseph Omog, mwalimu wa timu hiyo ameridhia usajili wa Kiemba. Mcameroon huyo sasa atakuwa na wigo mpana wa kufanya machaguo katika kikosi chake cha kwanza. Azam ilicheza kwa mara ya kwanza michuano ya CAF na kuishia hatua ya 16 bora, 2013, mwaka huu walishiriki kwa mara ya pili mfululizo michuano ya Shirikisho lakini hawakufanikiwa kuvuka raundi yoyote.
Wachezaji kama, Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Said Mourad, David Mwantika, Salum, Himid, Bolou, Domayo, Kipre Tchetche, nahodha, John Bocco, Wawa, Mcha Hamis, na wengineo hawana sababu nyingine ya kujitetea endapo watashindwa kuibeba timu hiyo kwa kukosa uzoefu. Wachezaji hawa hawatakiwi kuwa katika dhana ya mastaa na badala yake watapata mafanikio makubwa kama watachapa kazi kama walivyofanya wakati walipokuwa wakisaka taji la kwanza la Tanzania Bara msimu uliopita.
Kipre huwatewsa mabeki wa timu pinzani, Salum ni mchezesha timu wa aina yake, Bocco huzamisha mabao nyavuni. Azam ni timu ambayo wachezaji wake hutumia nguvu na akili, lakini timu nyingi makini pia ziko hivyo, kama watatumia nguvu nyingi kulinda lango lao itawasaidia sana, naKiemba ni mchezaji mgumu ambaye anaweza kushambulia na kuzuia akiwa katikati ya uwanja.
Hakuna mtu anayempa nafasi ya kutamba Kiemba katika timu ya Azam, lakini usajili huu umekuwa usio na mbwembwe, lakini una faida sana ndani ya malengo ya Omog na Azam FC kiujumla. Kiemba anaongeza namba ya wachezaji wa kuibeba Azam mwakani sambamba na Wawa na kiungo ambaye anarejea uwanjani Frank Domayo.