maneiva
Na BARAKA MBOLEMBOLE
Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Marcio Maximo tayari yupo nchini kuanza upya majukumu ya ufundishaji katika ardhi ya Tanzania. Maximo, amerudi Tanzania baada ya kuondoka nchini miaka minne iliyopita. Mchezo wake wa mwisho kama kocha wa Taifa Stars ulikuwa ni ule wa kichapo kutoka kwa timu ya Brazil katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kiungo hasiye na timu kwa sasa, Jabir Aziz alifunga bao pekee la Stars wakati ilipochapwa magoli 6-1, mwanzoni mwa mwezi juni, 2010 wakati Brazil ilipokuwa ikielekea katika fainali za kombe la dunia, nchini Afrika Kusini.
ALICHOKWA AU ALITUCHOKA?. 
Maximo aliamsha upya hali ya wapenzi wa kandanda nchini kuwa na uzalendo wa kuisapoti timu yao ya Taifa na alisisitiza mara zote kuwa Taifa Stars ni timu ya Watanzania na si yake. Alikuwa ‘ Mwalimu wa ndani na nje ya uwanja’, zaidi alionesha kujiamini katika kila maamuzi yake aliyokuwa akiyafikia kama mkuu wa benchi la ufundi. Alichagua kikosi kwa kufuata vigezo vya nidhamu, ubora, hali na hamasa ya wachezaji katika suala la uzalendo kwa timu yao ya Taifa. 
Mpango huo ulimletea mafanikio katika miaka yake mitatu ya mwanzo. Uteuzi wake wa kwanza wa kikosi cha Taifa Stars uliwashtua wengi. Alipokea timu iliyokuwa na zaidi ya wachezaji 30 kutoka kwa Mshindo Msolla. Maximo aliwashuhudia wachezaji wazuri akiwa jukwaani wakati Stars ilipolazimishwa sare na Rwanda katika uwanja wa Uhuru.
Aliwaacha baadhi ya wachezaji waliokuwa na majina makubwa wakati huo kutoka klabu za Simba na Yanga na kuwaita kikosini wachezaji chipukizi, kama Nidar Khalfan , Nadir Haroub ( ambao amekutana nao tena katika timu ya Yanga), Athumani Iddi, Henry Joseph, Kiggy Makasy, Amir Maftah ambao kwa kiasi kikubwa walimsaidia katika miaka yake mitatu ya mwanzo kama kocha wa Taifa Stars.
Tofauti nzake zisizokwisha na aliyekuwa kipa namba moja wa Tanzania, Juma Kaseja, na mitafaruku yake isiyokwisha na wachezaji muhimu wakati huo kama Athumani Iddi, Haruna Moshi, Maftah ilichangia kwa kiasi kikubwa kuondoka kwake kwani mashabiki wengi walikuwa upande wa wachezaji hao ambao walipoitwa kikosini na kocha aliyefuata, Jan Poulsen walifanikiwa kushinda kikombe cha Cecafa mwishoni mwa mwaka 2010 ikiwa ni miezi minne tangu kuondoka kwa Maximo ambaye mafanikio yake ya ndani ya uwanja yalikuwa kuifikisha Stars katika fainali za kwanza za CHAN, 2009.
Inawezekana alichokwa, lakini pia katika soka la Tanzania huwa hakuna uvumilivu. Makocha huondoshwa bila sababu za msingi, lakini kwa Maximo ilikuwa ni wazi Stars ilikuwa ikihitaji mwalimu bora zaidi yake ili kupiga hatua mbele. Bahati mbaya Jan na baadae Kim Poulsen walionekena kuishusha tena Tanzania badala ya kuipandisha. Maximo alituchosha wakati akiwa kocha wa Stars kutokana na kiburi chake, alikuwa kocha bora aliyeshindwa kupata mrithi sahihi Stars ndiyo maana ‘ tunasafa’ hadi sasa.
Kocha Mkuu mpya wa Yanga Marcio Maximo (kushoto)akiwa na Afisa Habari Baraka Kizuguto, Katibu Mkuu Beno Njovu na kocha msaidizi Leonadro Neiva mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa JK Nyerere jana mchana.
NDANI YA TIMU YA WANANCHI..
. Ukiniuliza iwapo, Maximo atafanikiwa ama laa! Katika klabu ya Yanga nitasema bila uoga wowote, Ndiyo. Maximo ni ‘ mtu hasa wa Yanga’, yupo ki-Yanga, Yanga katika mbinu za ufundishaji, stahili ya uchezaji na anaweza kwenda sambamba na mashabiki wenye presha na wasiopenda wachezaji wazembe katika timu yao. Mapokezi ambayo ameyapa wakati akiwasili nchi kwa kazi ya kuifunza Yanga yametoa ishara kuwa wapenzi wa soka nchini bado wana imani nae na wanathamini kile alichokifanya nchini katika kipindi chake cha miaka minne akiwa kocha wa Taifa Stars. 
Hamasa waliyonayo mashabiki wa Yanga imeonekana mara baada ya ujio wake. Ilikuwa ajiunge na klabu hiyo katikati ya Mwaka 2012 lakini dili hilo likashindikana. Akipenda kuichezesha timu yake katika mfumo wa kujinda na kushambulia kwa mashambulizi ya uhakika, Maximo atakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa katika msimu wake wa kwanza katika timu ya Yanga. Utulivu klabuni utakuwa ni jambo muhimu na anaweza kuifanyia mambo makubwa timu hiyo.
Afisa Haari wa Young Africans Bw Baraka Kizuguto (kushoto) akiwa pamoja na mshambuliaji mpya Andrey Coutinho mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa JK Nyerer leo
Kitendo cha kuambana na kiungo raia wa Brazil, Coutinho ni wazi kinamaanisha kuwa kocha huyo amejiandaa kuifanya Yanga kucheza soka la kumiliki mpira na kupata matokeo. Yanga ni timu inayohitaji matokeo kwanza kabla ya kiru kingine. Kostadin Papic, Sam Timbe, Tom Saintfiet, waliondoka Yanga baada ya timu kushindwa kupata ushindi katika ligi kuu. Wakati Walimu hao waliondolewa kwa sababu za matokeo mabaya katika ligi kuu, Dusan Kondic na Ernie Brandts wenyewe waliondolewa kwa sababu ya timu kushindwa kucheza mpira mzuri japo ilikuwa ikishinda.
Yanga wanataka nini?. Mashabiki wa timu hiyo siyo wavumilivu katika kila jambo. Kama kocha unahitaji kufanikiwa katika timu hiyo basi ni lazima ufanikiwe katika matokeo ya uwanjani na kucheza soka la kuvutia. Wakati anaondoka Tanzania kocha huyo alisema kuwa wachezaji wa Tanzania hawafundishiki. Sasa ni ubora gani ambao ataupata kutoka kwa wachezaji wa Yanga hilo ni jambo lingfine. Nyakati zinabadilika na inatubidi kuamini kuwa kila mtu hufanya makosa, pengine hata yeye alikuwa hashauriki ndiyo maana alishindwa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wachezaji.
Ni kocha ambaye ana uwezo mkubwa katika michezo ya michuano, hatujaona ubora wake katika ligi nap engine huko ana weza kuchanganyikiwa mambo yanapokwenda mrama. Nimefurahi kusikia kauli yake kuwa atamaliza tofauti zake zote na Kaseja na hivyo pia ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa kila mmoja ambaye anataka kuona mpira unaendelea nchini. Kupata mkufunzi kama huyu katika mpira wetu ni jambo la kuwashukuru viongozi wa Yanga na si kuanza kuhoji vigezo ambavyo vimetumika kumleta nchini kwa mara ya pili.

 
Top