Mbeya-City
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WASHINDI wa tatu wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita, klabu ya Mbeya City fc imeanza zoezi la kutafuta wachezaji wapya watakaosajiliwa kwa ajili ya kikosi cha pili.
Akizungumza na mtandao huu, katibu mkuu wa klabu hiyo, Emmanuel Kimbe amesema kuwa wachezaji wanaotakiwa ni kuanzia miaka 17 hadi 22 na zoezi hilo limeanza juzi na litafikia tamati juni 30 mwaka huu.
“Sasa hivi shughuli inayoendelea ni kufanya utambuzi wa baadhi ya wachezaji, lakini ni wachezaji wadogo wadogo wenye miaka 17 mpaka 22. Zoezi limeanza jana (juzi) saa tano litakwenda mpaka tarehe 30. Nia ni kupata wacheza watakaocheza kikosi cha pili na baadaye kikosi cha kwanza”. Alisema Kimbe.
Kimbe aliongeza kuwa baada ya zoezi hilo watakutana pande mbili za utambuzi kwa maana ya viongozi na benchi la ufundi ili kukamilisha usajili wa makinda hao.
Kuhusu asajili mwingine, Kimbe alisema utaendelea, lakini wanatarajia kusitisha kwasababu kwa kiasi kikubwa wachezaji wote wamebakia kikosini.
Kimbe alisema kwamba kikosi cha Mbeya City chini ya kocha bora wa msimu uliopita, Juma Mwambusi kitaingia kambini kuanzia julai 15 mwaka huu.
Hata hivyo aliongeza kuwa wanatarajia kucheza mechi za kirafiki nje ya nchi ili kujiweka sawa kwa msimu mpya unaotarajia kuanza kushika kasi mwezi agosti mwaka huu.
Msimu uliopita, Mbeya City ilimaliza nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 49 katika mechi 26 ilizocheza.
City ilishinda mechi 13, sare 10 na kufungwa mechi tatu dhidi ya Yanga sc, Coastal Union na mabingwa Azam fc.
Kikosi hicho cha Mwambusi kilitikisa nyavu mara 33 na nyavu zake kuguswa mara 20.
Licha ya matokeo hayo, Mbeya City iliifanya ligi kuu kuwa maarufu zaidi kutokana na ubora wake wa uwanjani na namna mashabiki wa soka wa jijini Mbeya walivyoungana kuisapoti timu yao.
Timu mbili zilizopanda na Mbeya City, Rhino Rangers na Ashanti United zilishindwa kuhimili mitanange ya ligi kuu na kushuka daraja.
Mbali na timu hizo, nao maafande wa JKT Oljoro walishuka daraja na kuzipisha timu za Stand United ya Shinyanga, Ndanda fc ya Mtwara na Polisi Morogoro ya Mkoani Morogoro
 
Top