Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WAKATA miwa wa Kaitaba, Kagera Sugar, rasmi wameanza kambi kujiwinda na mikikimikiki ya ligi kuu soka Tanzania bara inayotarajia kuanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange amezugumza na Mtandao huu na kufafanua kuwa jana walifika Bukoba kambini na leo hii ndio wameanza kusaka kasi mpya kuelekea msimu mpya.
“Mungu ametusaidia tumefika Bukoba kambini jana, kwahiyo leo tumeanza kambi yetu rasmi kujiwinda na ligi kuu”. Alisema Kabange.
Kabange aliongeza kuwa kusogezwa mbele kwa michuano ya ligi kuu ni faraja kwao kwani watapata muda mzuri wa kukijenga kikosi chao kilichosheheni vijana wapya.
“Ni kweli ligi imesogezwa mpaka septemba 20, kwa upande mwingine ni nafuu kwetu ili tuweze kujipangga vizuri”.
“kama unavyojua, tuna vijana wengi wapya, kwahiyo naona kwetu inakuwa faraja, tutaweza kuwaweka pamoja wachezaji wapya na wa zamani. Tunashukuru kwa kuweza kupata muda huu ulioongezwa”. Aliongeza Kabange.
Kuhusu matatizo ya kikosi chao msimu uliopita ambao walishika nafasi ya tano kwa kujikusanyia pointi 38, Kabange alisema: “Sisi tulikuwa na usumbufu zaidi katika safu ya ushambuliaji, kama ulivyo wimbo wa Taifa Tanzania, tumejitahidi kadri ya uwezo wetu kuchukua vijana chipukizi ambao wanaweza kutusaidia kama tulivyowatengeneza”.
“Them Felix `Mnyama` ameondoka kuelekea Mbeya City fc, tulikuwa na mpango na kocha wangu kuchukua mshambuliaji kutoka Uganda, lakini mipango hiyo imeshindikana. Kwahiyo wachezaji tuliowasajili ni Watanzania watupu na naamini tukifanya nao mazoezi tunaweza kufika pale tulipokusudia”. Alifafanua Kabange.