BARCELONA wanatarajia kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez ndani ya saa 48 zijazo.
Mazungumzo yanaendelea na miamba hiyo ya Hispania inataka kulipa moja kwa moja dau waliloambiwa juu ya nyota huyo mwenye miaka 27. Liverpool wanahitaji paundi milioni 80.
Licha ya kufungiwa miezi minne kucheza soka kwa kosa la kung`ata, Suarez ataruhusiwa kuchukua vipimo vya afya na tayari kamati ya nidhamu ya FIFA imethibitisha.
Mshambuliaji huyu wa Liverpool amefungiwa kujihusisha na shughuli zote za soka ikiwemo uwanjani, lakini haitamzuia kuhama klabu kama dili limekubaliwa
Mkuu wa kamati ya nidhamu ya FIFA, Claudio Sulser, alisema: “Mchezaji hawezi kufanya shughuli yoyote inayohusu mpira wa miguu, lakini vipimo vya afya kwa ajili ya uhamisho jibu ni ndiyo. Kifungo hakiingiliani na haki za uhamisho”
Suarez alikata rufaa dhidi ya kifungo chake cha miezi minne kwa kitendo chake cha kumng`ata mchezaji wa Italia, Giorgio Chiellini.
Kikao cha jumatano baina ya klabu mbili kilienda vizuri na kuna matarajio makubwa ya kufikia makubaliano.
Mkurugenzi mkuu wa Liverpool, Ian Ayre alikutana na maofisa wa Barca Raúl Sanllehí, Toni Rossich dona Jordi Mestre.