Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
UONGOZI wa Yanga sc umesema haumbanii winga wao hatari, Mrisho Khalfan Ngassa `Anko` kujiunga na klabu ya Free State Stars inayoshiriki ligi kuu nchini Afrika kusini.
Siku za karibuni kumekuwepo na taarifa za Ngassa kufanya majaribio na kufuzu katika klabu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Mbelgiji, Tom Saintfiet na kukubali kulipa dola elfu 80 ambazo ni sawa na milioni 130 za Kitanzania.
Lakini taarifa zinaeleza kuwa Yanga wamegoma kiasi hicho cha fedha na kusema wanahitaji dola laki moja na nusu sawa na milioni 240 za Kitanzani na ndipo Free State wametia ngumu juu ya kiasi hicho cha fedha.
Lakini inasemekana Free State ipo tayari kuongeza dau kidogo ili kupata huduma ya winga huyo mwenye kasi uwanjani.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu amesema hadhani kama uongozi unambania Ngassa kwani wakifuatilia kwa undani zaidi wanagundua kwamba kama unamtaka mchezaji duniani, sehemu yoyote, inageuka kuwa biashara, haigeuki kuwa ofa, haigeuki kuwa kubaniana ila ni biashara.
“Kama klabu ipo `serious` kumtaka, sioni kama kuna suala la kubaniana. Sidhani kama dau tunalosema ni kubwa kwa mchezaji kama Ngassa. Ni dau dogo sana kwa gharama ambazo tayari tumeshaingia kwake”. Alisema Njovu.
“Huwezi kufanya mambo bila kufuata taratibu za makubaliano.Tunafanya hivyo kwasababu sisi tunaelewa gharama ambazo tumeingia juu yake, tunaelewa kama kuna madeni yaliyopo yanayomhusu Ngassa, tunayajua, kwahiyo kuna vitu vingi sana vinatakiwa kuhusishwa kwenye hiyo hesabu, mtu wan je hawezi kujua”. Aliongeza Njovu.
Njovu alikanusha kusema wao wanataka kumuuza Ngassa kwasababu yeye ni binadamu, lakini wanajaribu kuzungumzia thamani yake.
Pia alisema wataongea na Ngassa akisharudi nyumbani akiwa katika majukumu ya kuitumikia timu ya Taifa, lakini tayari nyota huyo yupo nchini na jana alifika katika uwanja wa mazoezi wa Bandari Tandika akiwa amevalia nguo za nyumbani.
Mtakatifu Tom Saintfiet anaisaka saini ya Mrisho Ngassa katika klabu yake ya Free State Stars ya Afrika kusini.
“Sisi tunajua Ngassa yupo na timu ya Taifa, na kwasababu yupo na timu ya taifa, tunasubiri timu ya taifa irudi ili tuongee naye kama mchezaji, halafu tujue anaipimaje hiyo timu”. Alisema Njovu.
Aidha Njovu aliongeza kuwa wameikataza Free state kuongea na vyombo vya habari kwasababu haya ni mazungumzo ambayo yapo ndani ya klabu na sio vizuri kuongelea kwenye vyombo vya habari.
“Kama wao tumewakataza, basi nasisi hatupaswi kuongea hizo habari kwenye vyombo vya habari na hatutaki kutumia vyombo vya habari kufanya mazungumzo”.
“Tukimaliza mazunguzo ya ndani, hapo tunaweza kuzungumza kwenye vyombo vya habari”.
“ Hutajaweka kitu chochote kuwa kificho kwasababu hakuna kitu chochote kilichopo mezani, mpaka tupate vitu kamili na kuongea na watu ambao tunajua ni watu wanaohusika”.
“Bado hatujakaa mezani kuweza kuzungumza. Kwanza tunatakiwa kuongea na mchezaji, ngoja arudi kwanza kutoka timu ya Taifa baada ya kumaliza kazi hiyo tutamuulize”. Alihitimisha Njovu