Na Baraka Mpenja, Dar e salaam
MTIBWA sugar kila mwaka inabomolewa na timu nyingine za ligi kuu soka Tanzania bara kwa kuwasajili wachezaji wengi muhimu wanaong`ara klabuni hapo.
Kocha mkuu wa klabu hiyo, Mzalendo, Mecky Mexime amesema amejikuta kila mwaka anakuwa na kazi ya kujenga upya timu, kwasababu msimu unapoisha, wachezaji watatu au wanne wa kikosi cha kwanza wananunuliwa na timu nyingine zikiwemo Simba na Yanga.
“Timu nyingi zinaangalia kwetu Mtibwa, kila mwaka tunabomolewa, kila mwaka unajenga upya timu, kwasababu wanaondoka wachezaji watatu wanne, tena wachezaji muhimu”. Alisema Mexime.
“Sisi hatusajili wachezaji wa gharama, tunatafuta vijana wadogo na kuwajenga, lakini unakuta mwakani wamenunuliwa tena”.
Beki huyo na Nahodha wa zamani wa Mtibwa na timu ya taifa ya Tanzania , Taifa Stars alikiri kuwa kutengeneza upya timu ni jambo gumu, lakini amekuwa akijitahidi kila msimu kuja na vijana wapya.