Washambuliaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wanawasili nchini keshokutwa alfajiri (Julai 16 mwaka huu) kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji (Mambas).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika (AFCON) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Mambas itachezwa Jumapili (Julai 20 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ulimwengu na Samata watawasili saa 12 asubuhi kwa ndege ya EgyptAir wakitokea Tunisia ambapo timu yao ya TP Mazembe imepiga kambi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mahmoud Ashour kutoka Misri.
Stars itarejea jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa (Julai 18 mwaka huu) kwa ajili ya mechi hiyo wakati Mambas nao wanatarajiwa kutua siku hiyo hiyo. Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu nchini Msumbiji.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)