Na Baraka Mpenja
MABINGWA wa Tanzania, Azam fc wametupwa nje ya michuano ya kombe la klabu bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame kwa kufungwa penalty 4-3 dhidi ya El Merreik ya Sudan katika mchezo wa robo fainali.
Mshindi wa mchezo huo uliopigwa katika dimba la Nyamirambo mjini Kigali, Rwanda, alilazimika kupatikana kwa changamoto ya matuta baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana (0-0).
Mechi hiyo ilikuwa ngumu kwa timu zote kwani mashambulizi ya kupangwa yalitawala kwa pande zote.
Azam walikosa nafasi kadhaa za kufunga kupitia kwa washambulaiji wake,Kipre Herman Tchetche, John Bocco na Leonel Saint-Prexu, lakini nao Merreikh ambao wana historia kubwa katika soka la ukanda huu walishindwa kuzitumia vizuri nafasi walizopata.
Hata hivyo huwezi kuacha kumsifu kipa wa Azam fc, Mwadini Ali kwasabbau aliokoa michomo ya hatari langoni mwake ambayo ilikaribia kuingia nyavuni.
Penati tatu za Azam fc zilifungwa na beki wa kati Aggrey Morris, mshambuliaji alitokea benchi, Mrundi, Didier Kavumbagu na Erasto Edward Nyoni.
Beki wa kulia Shomari Salum Kapombe na Mshambulaiji, Mhaiti, Leonel Saint- Prexu alikosa penalti yake.
Kwa matokeo haya, Azam fc kesho wanasafiri kurudi Dar es salaam Tanzania,wakati Merreikh wanamsubiri mshindi wa mechi ya pili inayoendelea muda huu baina ya KCC ya Uganda na Altabara ya Sudan kusini.
Nusu fainali moja imeshajulikana ambapo timu mbili za Rwanda, Polisi na APR zitachuana baada ya kushinda kwa penalti pia katika michezo ya jana.
Polisi waliifunga Atletico kwa penati 9 kwa 8, wakati APR waliitoka Rayon Sport kwa penalti 4 kwa 3