Kocha mkuu wa Simba sc Patrick Phiri akiongea na wachezaji wake
Baraka Mpenja, Dar es salaam
RATIBA ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2014/2015 utakaoanza kutimua vumbi septemba 20 mwaka huu umeanikwa hadharani na Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF.
Afisa habari na mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura Mgoyo katika taarifa yake amesema ratiba hiyo imezingatia michuano ya Chalenji itakayochezwa Novemba, usajili wa dirisha dogo Nov 15- Des 15, ushiriki wa klabu za Azam na Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa (CL) na Kombe la Shirikisho (CC).
Wambura alisema mechi zitachezwa wikiendi ili kuongeza msisimko/kuwapa fursa washabiki wengi zaidi kuhudhuria, na katikati ya wiki imeachwa wazi kwa ajili ya mechi za Kombe la FA (Federation Cup).
Vilevile kutakuwa na mechi Boxing Day na siku ya Mwaka Mpya.
Siku ya ufunguzi zitapigwa mechi saba katika viwanja tofauti nchini ambapo mabingwa watetezi Azam fc wataanza kutetea ubingwa wao dhidi ya wageni Polisi Morogoro katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es saalam.
Yanga chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo wataanza ugenini katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar.
Timu mbili zilizopanda ligi kuu msimu huu, Stand United na Ndanda fc zitachuana katika dimba la Kambarage mkoani Shinyanga.
Mgambo JKT watakawakaribisha Kagera Sugar katika dimba la CCM Mkwakwani jinni Tanga.
Ruvu Shooting wataanza kampeni zao katika uwanja wao wa Mabatini uliopo Mlandizi Pwani dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.
Wagonga nyumbo wa Mbeya City fc wataanza nyumbani katika dimba la CCM Sokoine Mkoani Mbeya dhidi ya JKT Ruvu.
Wekundu wa Msimbazi Simba chini ya kocha Mzambia, Patrick Phiri wao wataanza kampeni za kuusaka ubingwa wa ligi kuu bara septemba 21 dhidi ya Coastal Union uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Raundi ya pili itacheza septemba 27 na 28 mwaka huu ambapo timu zote zitashuka dimbani.
Septemba 27, wekundu wa Msimbazi Simba watacheza mechi yao ya pili nyumbani dhidi ya Polisi Morogoro.
Mechi nyingine siku hiyo zitakuwa baina ya Mtibwa Sugar dhidi ya Ndanda fc katika uwanja wa Manungu Turiani. Azam watawakaribisha Ruvu Shooting Chamazi, Mbeya City watachuana na Coastal Union uwanja wa Sokoine, wakati Mgambo JKT watakuwa Mkwakwani kuchuana na Stand United.
Raundi ya pili itakamilika septemba 28 ambapo JKT Ruvu watavaana na Kagera Sugar katika uwanja wa Azam Complex.
Mechi nyingine itawakutanisha Yanga sc ya Maximo dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Endelea kufuatilia mtandao huu kwasababu utaendelea kukujuza kuhusu ratiba nzima ya ligi kuu soka Tanzania bara.