MLINDA mlango namba moja wa Simba sc, Ivo Philip Mapunda amepania kufanya makubwa katika msimu mpya wa ligi kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi Septemba 20 mwaka huu.
Simba chini ya kocha mkuu, Mzambia, Patrick Phiri akisaidiwa na kiungo wa zamani wa klabu hiyo na timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ itaanza kampeni ya kusaka ubingwa dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union, Septemba 21 mwaka huu uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Akizungumza na MPENJA BLOG mchana huu, Ivo amesema kocha Patrick Phiri ameleta mabadiliko makubwa katika kikosi cha Simba na wanatarajia kushirikiana naye ili kufikia malengo yao.
Ivo aliongeza kuwa wakati wa utawala wa Mcroatia, Zdravko Logarusic, wachezaji walikuwa na mipaka ya kucheza mpira na hawakutumia vipaji vyao kwa uhuru, lakini kwa kocha Phiri mambo ni tofauti kwasababu wachezaji wanafanya kile wanachoweza na kuonesha vipaji kwa uhuru.
Kipa huyo mkongwe aliyewahi kucheza Yanga na Gor Mahia ya Kenya alisema kwamba mchezo wa mpira wa miguu ni mchezo ambao unatakiwa kucheza vile ambavyo unajua, halafu baadaye  unaongeza vitu vingine kutoka kwa mwalimu.
“Tunachotarajia ni kufanya vizuri kwasababu mwalimu aliyekuja nadhani kwa namna moja ama nyingine ameleta mabadiliko. Simba ambayo iliyokuwepo msimu uliopita na ya sahizi ni tofauti, ukiangalia mechi tulizofanya majaribo tumefanya vizuri”. Alisema Ivo.
“Timu inafanya vizuri kutokana na kwamba mwalimu anajaribu kuwapa wachezaji uhuru wa kufanya kile kinachowezekana uwanjani. Unajua Uwanjani unapompa uhuru mchezaji, nadhani anacheza vizuri bila wasiwasi,”.
”Alipokuwepo Mwalimu Logarusic nadhani kulikuwa na mipaka fulani ambayo lazima mchezaji ufuate na usipofuata anakuwa mkali na wachezaji walikuwa wanapoteza kujiamini”.
Mlinda mlango Ivo Mapunda enzi za utawala wa kocha Zdravko Logarusic
“Kwahiyo nategemea kwamba tutafanya vizuri na lengo letu ni kuleta mabadiliko ambayo lazima tushike nafasi ya kwanza katika msimu wa ligi ambao utaanza hivi karibuni,”.
Kuhusu kusajiliwa kwa kipa bora wa msimu uliopita, Hussein Shariff ‘Casillas’ kutoka Mtibwa Sugar, Ivo alisema ni changamoto nzuri kwake kwasababu anaamini kuna vitu vipya atavichukua kwa kipa huyo kijana hali kdhalika naye atajifunza kutoka kwake kutokana na uzoefu alionao.
 “Changamoto katika nafasi ya golini zipo. Unajua changamoto zinakuja pale unapofanya vibaya na hiyo nafasi mwingine anaitolea macho. Kinachofanyika zaidi ni mazoezi ya ziada na utulivu unapokuwa kwenye mchezo ili kupunguza makosa ambayo mwingine hawezi kuyafanya”.
“Kitu kikubwa kinachoweza kunifanya pengine nionekane kama nacheza  vizuri ni jinsi ya kuongea na wachezaji kadri mchezo unavyoendelea,”
“Kutokana na uzoefu wangu najua nini cha kufanya pindi mchezo unapoendelea. Nakuwa nausoma mchezo na kujua nifanye nini ili tuweze kukwepa madhara ambayo yakitokea watu wataangalia golikipa alikuwa ni nani.”
“Uwepo wa golikipa mwingine Casillas nadhani itanisaidia mimi. Unapokuwa na mtu mwingine tofauti toka timu nyingine, unajifunza kitu kingine. Kama kipa huwezi kujua kila kitu, kwahiyo unaweza kujifunza kutoka kwa kipa anayechipukia hata kama ni kipa mzoefu”.
“Hivyo Casillas ananisaidia mimi tunapokuwa mazoezini au atakapokuwa anacheza mechi nitajifunza kwake na yeye anajifunza vitu kutoka kwangu”.
Simba chini ya uongozi mpya unaoongozwa na Rais Evans Elieza Aveva wamepania kufuta machungu ya kufanya vibaya kwa miaka mitatu mfululizo.
Ili kuhakikishwa wanafanya vizuri, kamati ya usajili chini ya ‘Big Boss’. Keptein wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe, imefanya usajili makini.
Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa na Simba ni Emmanuel Okwi, Pierre Kwizera, Pual Kiongera, Shaaban Kisiga, Abdi Banda, Joram Mgeveke na wengineo.
 
Top