Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Unamkumbuka, Ruud Voller?. Hata kwa kutazama video zake za miaka ya nyuma. Voller alifunga bao la ushindi katika mchezo wa fainali za kombe la dunia, mwaka 1990 wakati Ujerumani ilipoishinda Argentina kwa mabao 2-1.
Enzi za uchezaji wake mashabiki wa soka nchini Ujerumani walimpachika jina la ‘ bingwa wa magoli yasiyovutia duniani’. Magoli ya Voller yalikuwa hayasisimui kama magoli yanayofungwa na akina Cristiano Ronaldo, Zlatan Ibrahimovic, Neymar, Leonel Messi.
Kilichovutia katika moyo wa Voller ni kuhakikisha anafunga mabao kadri inavyowezekana na kuisaidia timu yake kushinda mataji. Jina halitafutika kamwe kwa kile alichoifanyi nchi yake, rekodi yake ya mabao katika ligi ya Bundesliga bado inasomeka na sifa yake ni ileile hadi sasa, ‘ bingwa wa mabao yasiyovutia duniani’.
Ulimuona mshambulizi, Geilson Santos ‘ Jaja’ katika mchezo wa jana wakati timu yake ya Yanga ilipofanikiwa kupata ushindi ‘ mwembamba’ wa bao 1-0 dhidi ya Thika United ya Kenya katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki?. Je ni mchezaji wa aina gani? Ataisaidia Yanga? Kuna baadhi ya mashabiki walionekana kumzomea mshambulizi huyo kutoka Brazil wakati mchezo ukiendelea, lakini dakika 15 baada ya kuanza kipindi cha pili mchezaji huyo akawanyamazisha kwa bao la ‘ kujituma’ akiwahi katika nafasi ambayo krosi ya Saimon Msuva ilikuwa ikikatiza.
MCHEZAJI MVUMILIVU
Jaja ni mzito, mwili wake wenyewe ni mzito lakini goli lake limekumbusha kitu muhimu kuwa uzito wake haupo hadi katika kujipanga na kutumbukiza mpira nyavuni. Akili yake ina uharaka na mchezaji ambaye anafikia maamuzi ya kujaribu kufunga hata kama sehemu aliyopo ni ngumu. Hakuwa na lolote katika kipindi chote cha kwanza lakini aliwafanya viungowanne wachezesha timu kuwa huru. Alijitahidi kuituliza mipira na kupiga pasi kwa wenzake, kitu kingine alionyesha namna anavyoweza kutumia uzito wake kuwabana walinzi wa timu pinzani.
Haijalishi kama bao lake ni la kuvutia ama sivyo, lakini kilicho bora ni kwamba alifunga bao akicheza kama mshambulizi huru kwa dakika 87 na kutimiza jukumu hilo ipasavyo. Mwalimu Maximo alimvumilia mchezaji huyo licha ya kukutana na changamoto za kuzomewa katika kipindi cha kwanza. Na jambo hilo lilimfanya mchezaji huyo kuendelea kucheza kwa kujiamini. Mchezaji pia alionyesha uvumilivu kutokana na kile alichokishuhudia katika baadhi ya majukwaa. Maximo ameanza vizuri.
JAJA KUFUNGA KATIKA UWANJA WA TAIFA KATIKA MCHEZO WAKE WA KWANZA.
Ni kitu kizuri kwa mchezaji mpya kufunga mbele ya mashabiki wa klabu yako katika mchezo wa kwanza ndani ya uwanja wa nyumbani. Wakati kocha wake akifurahia na kufanikiwa kwa mbinu zake, Jaja amefanikiwa kufanya vizuri licha ya kwamba si kwa kiwango cha juu. Ingekuwa si vizuri kushindwa kufunga wakati nyuma yake alichezeshwa Msuva, Haruna Niyonzima akicheza kama kiungo mchezesha timu akitokea katikati ya uwanja, Hassan Dilunga akichezesha timu akitokea upande wa kulia na Countinho akifanya hivyo akitokea upande wa kushoto.
Viungo hao wanne wote ni wachezesha timu wazuri hivyo hakukuwa na sababu ya Jaja kucheza dakika 87 bila kufunga. Ametoa zawadi nzuri kwa mashabiki wa timu yake. Mabao mawili katika michezo minne, bila shaka ataendelea kufunga zaidi katika ligi kuu. Jaja si Voller ila anaweza kufunga zaidi mabao kama ilivyokuwa kwa kina Ambani Boniface na Maurus Sunguti, Yanga haijawahi kuwa na mshambulizi wa kuvutia ila daima wametoa wafungaji bora wa ligi kuu Bara mara kibao, sijui kwa Jaja ila ataendelea kuwafunga magoli yasiyovutia na atajiwekea sifa yake kama Ambani kama amtamuheshimu.