Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MLINDA mlango mkongwe nchini, Juma Kaseja anatarajia kusimama katika milingoti mitatu, Yanga ikiikabili Big Bullets FC (zamani Bata Bullets) ya Malawi ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Hali hiyo inatokana na mlinda mlango namba moja wa klabu hiyo, Deogratius Munish kuwa katika majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars , itakayocheza mechi ya kimataifa ya kirafiki iliyopo katika kalenda ya FIFA dhidi Burundu kesho mjini Bujumbura.
Kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali ‘Mensah’ amesema Yanga ina makipa watatu wenye kiwango cha kuu na yeyote yule anaweza kufanya kazi nzuri uwanjani.
“Siri yetu sisi ni kwamba makipa wetu watatu, Juma Kaseja, Ally Mustapha na Deogratius Munish ‘Dida’ wanafanya mazoezi katika kiwango cha juu na ni makipa bora”.
“Mifano iko hai, katika mchezo iliofanyika Pemba tulishinda bao 1-0 na kule Ungaji kila tulipocheza tulishinda 2-0. Matokeo haya yanaonesha makipa na safu ya ulinzi wako sawasawa,”
“Makipa wangu wote wako katika kiwango cha kufanana.Hatuna matatizo katika mchezo wa kesho kwasababu makipa wanafanana. Hata kule Zanzibar mwalimu Maximo alikuwa anatoa timu nzima, anaanzisha golikipa na timu yake nyingine”.
Katika kikosi cha pili cha Yanga mara zote langoni anasimama Kaseja, hivyo ni dalili tosha kuwa kesho ndiye atakayeanza kama hatakuwa na tatizo lolote.
Tayari Big Bullets wameshatua Dar es salaam na maandalizi kwa ajili ya mechi yamekamilika.
Afisa habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema wachezaji wote wapo katika morali ya juu na mechi hiyo inatarajia kuanza majira ya saa 10:00 jioni kwa mujibu wa waandaaji wa mechi DRFA.