Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa
Stars) inashuka uwanjani Oktoba 12 mwaka huu kuikabili Benin katika mechi ya
kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Programu ya Taifa Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kwa ajili ya mechi hiyo itatangazwa
baadaye na Kocha Mkuu Mart Nooij.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linaendelea na taratibu nyingine kwa ajili ya mechi hiyo ikiwemo
usafiri wa Benin kuja nchini, ambapo timu hiyo inatarajiwa kutua Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Oktoba 10 mwaka huu ikiwa na
msafara wa watu 28.
Pambano la Stars na Benin
litatanguliwa na mechi ya kudumisha upendo kati ya viongozi wa dini ya Kikristo
na Kiislamu.
Wakati huo huo, kutokana na mechi
hiyo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inafanyiwa marekebisho madogo, na
marekebisho hayo yatatangazwa kesho (Septemba 26 mwaka huu).