MABEKI Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Aggrey Morris na kipa Mwadini Ali, wamerejeshwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar, ‘Zanzibar Heroes’.
Akitangaza wachezaji watakaofanya mazoezi kwa ajili ya kupata kikosi kitakachoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu yatakayofanyika nchini Ethiopia, kocha mkuu wa timu hiyo Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema kuwa amewateua wanandinga hao na wengine waliotemwa mwaka jana ili kurejesha mshikamano.
Morocco, kocha wa zamani wa Coastal Union ya Tanga, ametangaza wachezaji 36 ambao watafanya mazoezi na baadaye kuchujwa ili kupata 20 wa mwisho watakaopeperusha bendera ya Zanzibar kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Hata hivyo, amesema haikuwa kazi rahisi kufanya uteuzi huo, na alilazimika kufanya ziara katika visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Tanzania Bara ili kuangalia na kujiridhisha viwango vya wachezaji hao.
Amesema kigezo kingine alichozingatia, ni iwapo wachezaji hao wanapata nafasi ya kuzichezea klabu zao kwenye mechi za ligi na nyinginezo.
Wachezaji hao na timu wanazotoka kwenye mabano kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa leo kwenye mtandao rasmi wa Azam FC ambayo imetoa wachezaji watano, ni makipa; Mwadini Ali (Azam), Khalid Mahadhi (Mafunzo), Mudathir Yahya (KMKM) na Mwalimu Ali (Prisons).
Mabeki; Mohammed Othman (Polisi), Said Mussa (Mafunzo), Shafii Hassan (Zimamoto), Ismail Khamis (JKU), Adeyoum Saleh (Chuoni), Edward Peter (Hard Rock), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga), Nahoda Bakari (Polisi Moro), Aggrey Morris na Abdallah Sebo (Azam), Nassor Masoud ‘Chollo’ na Abdulaziz Makame (Simba SC), Mohammed Faki ( JKT Ruvu) na Khamis Ali (KMKM).
Viungo ni Mohammed Issa (Chuoni), Mohammed Abdulrahim, Ali Juma (Mafunzo), Amour Suleiman (Malindi), Makame Hamad (Zimamoto), Awadh Juma (Simba), Khamis Mcha ‘Vialli’, Mudathir Yahya (Azam), Abdulhalim Humoud (Sofapaka-Kenya) na Suleiman Kassim ‘Selembe’ (Polisi Moro).
Washambuliaji; Omar Juma (Hard Rock), Mohammed Seif (Dogomoro), Fasihi Hija (Malindi), Simai Masoud (Fufuni), Nyange Othman, Ibrahim Hilika (Zimamoto), Said Juma ‘Kizota’ (Yanga) na Ame Ali (Mtibwa Sugar).
Kocha huyo ametaja mikakati ya mazoezi kwamba ameigawa katika sehemu mbili, akianza na wachezaji waliopo Zanzibar na baadaye atajumuisha walioko nje ya Zanzibar wakati ligi zitakaposimama.
Hata hivyo ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu haitoi nafasi ya kusimama zaidi ya kupisha michuano ya Chalenji na mechi nyingine za timu za taifa.
Amefahamisha kuwa, awali alipanga kuanza mazoezi mwezi huu wa Oktoba, lakini hilo limeshindikana na badala yake itakuwa Novemba mosi.
Morocco ameeleza kuwa tayari amekiagiza Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kujaribu kutafuta mechi za kirafiki ili kujipima nguvu.
Naye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA Masoud Attai, amesema kuwa, tayari wameshatuma barua nchi za Kenya na Uganda kupitia vyama vyao vya soka kuomba mechi hizo na kinachisubiriwa ni majibu.
Attai amewaomba wafanyabiashara mbalimbali kujitokeza kuisadia timu hiyo, ili iweze kujiandaa vyema kwani inahitaji fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi.
picha juu ni aggrey morris akiwa na timu yake ya zanzibar