kocha
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Kiwango cha Simba SC katika mchezo dhidi ya mahasimu wao Yanga SC wiki iliyopita kimeoneka ‘ kulituliza’ jiji la Dar es Salaam. Kuelekea mchezo huo siku ya Jumamosi asubuhi mashabiki wa soka ‘ walitanda’ kila barabara ambazo zinaelekea uwanja wa Taifa, katikati ya mji, mashabiki wa Yanga walikuwa wakicheza ngoma, nyimbo huku wakiimba kwa furaha. Walikatiza kando ya jingo la makao makuu ya klabu ya Simba. Ilikuwa rah asana na muendelezo wa mvuto wa mechi ya Simba na Yanga uliendelea kuwepo licha ya upande wa Simba kuonekana si bora kwa miezi saba sasa.
Kuna tofauti kubwa kutoka michezo mitatu ya mwanzo ya msimu na huu uliopita ( dhidi ya Yanga)” anasema kocha wa Simba, Patrick Phiri ambaye anasema makosa ya nyuma yamechangia kuwa katika nafasi mbaya. Simba walimiliki mpira kwa muda mwingi, wakicheza huku wakionekana ‘ wakakamavu’, lakini uwezo wao mdogo kimbinu ulifanya washindwe kutengeneza nafasi za kutosha licja ya mara mbili mshambulizi, Elius Maguli kuonekana akikosa mabao ya wazi.
Yanga walikuwa na mbinu bora za kujilinda licha ya kuzidiwa katika ufundi na ‘ kundi la yosso ‘ ambalo Phiri aliammua kulianzisha; “ Tunatakiwa kuendelea kucheza hivi dhidi ya Prisons na Mtibwa Sigar. Tulijilinda vizuri katika mchezo dhidi ya Yanga, tulipanga mashambulizi, lakini kuumia mapema kwa baadhi ya wachezaji kulivuruga mipango yetu lakini bado vijana walicheza vizuri ingawa hatukupata ushindi” anasema kocha huyo ambaye ameshinda michezo minne dhidi ya Yanga, akipoteza mara moja na kwenda sare mara sita katika vipindi tofauti akiwa kocha wa Simba.
Baada ya kucheza michezo minne mfululizo katika uwanja wa nyumbani na kuambulia pointi moja, Simba itasafiri kucheza na Tanzania Prisons siku ya Jumamosi ijayo katika uwanja wa Sokoine ambako hawakupata pointi yoyote msimu uliopita. Mchezo wa msimu uliopita kati ya Prisons na Simba katika uwanja huo ulimalizika kwa suluhu ya bila kufungana, pia ikumbukwe, Simba walilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Mbeya City katika uwanja huo. Mara baada ya mchezo huo ‘ Wekundu wa Msimbazi’ wataenda Morogoro kucheza na Mtibwa . Sehemu ngumu kwa timu za Dar es Salaa.
“ Ligi ni ngumu, kucheza nyumbani kuna faida kubwa lakini hakuna sababu ya kutoshinda ugenini kama una tomu bora. Tunatakiwa kuendelea kupandisha kiwango chetu, tuendelee kucheza kama tulivyocheza dhidi ya Yanga huku tukipandisha kiwango. Tulicheza vibaya katika michezo iliyopita, hatutakiwa kucheza hivyo tena.”
 
Top