Na Shaffih Dauda,
Katika soka la Tanzania wachezaji ndiyo huwajibishwa pindi timu inapofanya vibaya uwanjani na si makocha kama ilivyo kwa nchi za wenzetu. Popote pale duniani timu inapofanya vibaya, Walimu na benchi zao za ufundi ndio hufukuzwa kazi. Jambo hilo halipo! Mchezaji hawezi kutuhumiwa kwa kusikia maneno au kutokana na mahusiano ya ‘mtu na mtu’. Hii ni tabia mbaya, ni ‘ uswahili ambao ndani yake unabeba chuki za wazi’..
Matokeo mabaya ya timu katika michezo mitano ya mwanzo msimu huu katika ligi kuu yamehusika kuwaweka wachezaji hao (Kiemba,Chanongo na Kisiga ) katika ‘ lawama’, lakini ukweli zipo sababu za msingi ambazo si za kimpira zilitotumika kuwahukumu .
Mara nyingi tumekuwa tukisisitiza klabu kuwa na uwezo wa ‘ kuwasajili na kuwamiliki’ wachezaji kwa kutumia vyanzo vyao vya mapato. Poppe ametumia nafasi yake mara kadhaa kuonyesha chuki kwa baadhi ya wachezaji , Kuna wakati alihoji hadharani kwa nini Kiemba anapangwa katika kikosi cha Samba! Kwa kiongozi hiyo si kauli ya kuongea katika vyombo vya habari. Tazama siku chache baada ya kiongozi huyo kutoa maneno hayo, Kiemba amesimamishwa, si yeye tu,
Chanongo amekuwa ‘ akisingiziwa tu’ kuwa ‘ yeye ni Yanga’, huo ni uswahili. Kuna ushahidi gani wa kuthibitisha hilo?. Sababu kubwa iliyofanya Kiemba, Chanongo na Kisiga kusimamishwa ‘ ni kutumika’, kwa maana ya kuihujumu timu yao ifungwe. Katika hali ya kawaida hadi kufikia hatua ya kuwasimamisha ilipaswa uwepo ushahidi, na si kufanya uamuzi mkubwa kwa sababu za ‘ maneno ya kusikia mitaani’. Kelele za mashabiki kusema wachezaji hao wanacheza chini ya kiwango si sababu ya maana. Simba ina wachezaji wangapi?
Katika orodha ya wachezaji zaidi ya 25 kwa nini kocha aamue kumtumia Chanongo pekee?. Labda kama wachezaji wote katika timu hawana uwezo ndiyo maana kocha anaamua kumtumia Chanongo. Hili ni tatizo la viongozi wengi katika soka la Tanzania ambao njia zao za kuingia madarakani huwa si sahihi. Kuchaguliwa bila sera hupelekea kuingia madarakani watu wenye hela, ambao wanapofika katika nafasi hizo huwashinda sababu ya kukosa ‘ sifa ya wanachokisimamia’.
Zamani enzi zile Simba ikiwa na ‘ makomandoo’ mambo kama hayo yalikuwa yakifanyika, lakini katika zama za sasa ambazo mchezaji anasainiwa kwa mkataba, akilipwa mshahara, atawezaje kuhujumu kazi yake ambayo inamfanya mtu kama Kiemba mwenye mke na watoto? . Hili haliwezi kuingia akili mwa mtu mwenye ‘ fikra chanya’.
Huku ni kubomoa badala ya kujenga. Popote pale duniani timu inapofanya vibaya, mtu anayewajibika ni mwalimu na benchi lake la ufundi na si mchezaji hata siku moja. Wachezaji wangapi watafukuzwa kwa mtindo huo. Chanongo anasimamishwa mara ya ngapi sasa? Kwa nini inakuwa hivyo?. Mchezaji alicheza vizuri ‘ inakuwa poa’, akishuka kidogo kiwango ‘ anahujumu’!!!